MWANASOKA bora wa zamani wa dunia,
Mreno Luis Filipe Madeira Caeiro Figo
anatarajiwa kutua kesho na msafara wa
kwanza ya magwiji wa Real Madrid tayari kwa
mchezo dhidi ya magwiji wa Tanzania Agosti
23 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Figo ataongozana na nyota wengine wawili
waliowika Real Madrid muongo uliopita,
mshambuliaji Michael Owen aliyeshinda tuzo
ya mchezaji bora chipukizi Kombe la Dunia
mwaka 1998 Ufaransa na mwanasoka bora wa
Oceania mara mbili 1995 na 1998 Christian
Karembeu.
Figo aliyestaafu Mei 31 mwaka 2009, alipiga
tuzo mbili mfululizo mwaka 2000, Mwanasoka
Bora Ulaya na Dunia na anakuja Tanzania
kuwakumbushia watu enzi zake anatamba Real
Madrid.
Mapokezi makubwa yameandaliwa kwa ajili ya
magwiji hao Real Madrid ambao sasa wanakuja
kwa awali na hadi Agosti 22 kikosi kizima
kitakuwa kimekamilika Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa makampuni ya Tanzania Sisi ni
Nyumbani (TSN), Farough Baghozah
ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba magwiji hao
watapokewa kwa maandamano Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Dar
es Salaam na kupelekwa hoteli ya Ladger
Plaza, Bahari Beach.
Kikosi cha magwiji wa Tanzania,
kitakachomenyana na Real Madrid kinaendelea
mazoezi Uwanja wa Karume kwa wiki sasa kwa
ajili ya mchezo huo wa kihistoria.
Makipa maarufu waliowahi kuwika nchini,
Mwameja Mohamed na Manyika Peter
wamejumuishwa katika kikosi cha Tanzania All
Stars kitakachomenyana na magwiji hao wa
Real Madrid.
Chini ya makocha Charles Boniface Mkwasa
‘Master’ na Wasaidizi Freddy Felix Minziro na
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Daktari Mwanandi
Mkwankemwa na viongozi Mtemi Ramadhani,
Hassan Mnyenye, Omar Gumbo na Hamisi
Kisiwa kikosi hicho kitaingia kambini Dar es
Salaam kujiandaa kwa mchezo huo wa Agosti
23, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wengine walioItwa ni mabeki Nsajigwa
Shadrack, Mecky Mexime, Boniface Pawasa,
John Mwansasu,
Abubakar Kombo, George Masatu, Habib
Kondo,
Viungo Suleiman Matola, Shaaban Ramadhani,
Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’,
Yussuf Macho, Abdul Mashine, Abdul Maneno,
Mao Mkami, Steven Nyenge, Madaraka
Suleiman, Akida Makunda na Mtwa Kihwelo.
Washambuliaji ni Monja Liseki, Iddi Moshi,
Dua Said, Emmanuel Gabriel, Said Maulid,
Thomas Kipese, Nasor Mwinyi ‘Bwanga’,
Edibilly Lunyamila, Mohamed Hussein
‘Mmachinga’, Clement Kahbuka,
Madaraka Suleiman na Akida Makunda.
Wachezaji waliotamba kuanzia La Liga,
wakacheza ligi nyingine za Ulaya, Kombe la
Ulaya, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia
waliowahi kuchezea Real Madrid watakuja
nchini.
Katika ziara hiyo, pamoja na kucheza mchezo
wa kirafiki na kikosi maalum cha wachezaji
nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya
utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo
kupanda mlima Kilimanjaro.
Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja na
Real nchini ni pamoja na Wanasoka Bora wa
zamani wa Dunia, Mfaransa Zinadine Zidane,
Mreno Luis Figo na Mbrazil, Ronaldo Lima. Na mdadisiblog,/festosaimon |