Wednesday, November 19, 2014

Njia 5 za kumrudisha mpenzi wako baada ya kuzinguana

Katika uhusiano kunaweza kutokea ugomvi ambao ni wa kawaida na ambao hauhitaji nguvu kubwa kuumaliza lakini upo ule ambao ukitokea ni lazima nguvu ya ziada itumike ili kuweza kurudi katika mazingira ya amani na furaha.
Kutokana na hilo, leo nimeona nizungumzie mbinu tano zinazoweza kukusaidia katika kumrudisha mpenzi wako ambaye mmezinguana lakini bado unampenda.
Kumbuka wapo ambao wanagombana na inakuwa ndiyo mwisho wa uhusiano kutokana na ukweli kwamba hawakuwa wakipendana kwa dhati.
Lakini kwa wewe ambaye unampenda huyo uliyenaye lakini ikatokea kwa namna moja au nyingine ukamzingua, mambo haya matano yatakusaidia katika kumrudisha kwenye penzi lenu.

Kwanza, fanya kila unavyoweza ujue chanzo cha kutofautiana na kufikia hatua ya kugombana. Ukweli ni kwamba, ili kulitatua vizuri tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo chake. Ukishindwa kugundua chanzo cha tatizo, basi na wewe unakuwa sehemu ya tatizo.
Utashangaa wapenzi wengi hugombana na mambo kuwa makubwa kabisa kwa sababu ya mambo madogomadogo ambayo walishindwa kuyagundua mapema na matokeo yake yanazaa tatizo kubwa sana.

Pili, muache kwanza hasira zake ziishe. Kila binadamu ameumbwa akiwa na hasira na kwa bahati mbaya ni wachache wanaoweza kuzidhibiti. Ni rahisi mtu kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na hasira.
Baada ya kugombana, kila mmoja lazima atakuwa na hasira na njia pekee inayoweza kuepusha matatizo zaidi, ni kujipa muda na kumpa muda mwenzako ili hasira ziyeyuke.
Ukishaona hasira zenu zimekwisha hapo sasa unaweza kuanzisha mada juu ya kilichosababisha mkagombana. Tumia lugha ya upole kwani endapo utakuwa ukifoka au kuzungumza kwa jaziba, huwezi kuondoa tatizo badala yake itakuwa ni kama unaliongeza.

Tatu, mpe uhuru wa kuzungumza. Huwezi kumuelewa mtu kabla hujampa nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile alichokusudia kukisema. Endapo tatizo limetokea na upo kwenye hatua za kusaka amani, mpe mwenzako nafasi ya kueleza dukuduku alilo nalo.

Usimkatishe wala kumbishia chochote, muache aongee ulichomuudhi mpaka dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze kwa ustaarabu.

Nne, itakuwa vyema ukaomba msamaha. Hakuna silaha nzuri inayoweza kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutuliza mambo kabla hayajawa mabaya kama kuomba msamaha.

Hata kama unaona dhahiri huna makosa, omba msamaha kwanza kisha baada ya hapo anza kumuelewesha ‘mtu’ wako kwa upole. Lazima mwisho na yeye atayaona makosa yake na kukuomba msamaha, mtaweza kuepuka kuukuza ugomvi huo.

Tano, usiweke kinyongo. Endapo umeamua kuomba msamaha kwa mpenzi wako, au yeye amekuomba msamaha, samehe kwa dhati kutoka ndani ya moyo wako na sahau kile kilichotokea.

Ukisamehe kwa dhati, jifunze na kusahau kwani kusamehe kunaenda sambamba na kusahau. Elewa kwamba mpenzi wako ni binadamu ambaye hajakamilika, wala si malaika.Lazima atakuwa akikosea mara kwa mara, endapo utakuwa ukilimbikiza vinyongo, unafuga matatizo makubwa kwani siku nyingine akikukosea hata jambo dogo, utakumbushia na ya jana na juzi na mwisho ugomvi utakuwa mkubwa sana.

Nihitimishe kwa kusema tu kwamba, walio kwenye uhusiano ni sawa na vikombe vilivyo kabatini, yaani kugongana ni kitu cha kawaida. Cha msingi ni wapenzi kujua njia sahihi za kuondoa tofauti zao na kuendelea kuishi maisha yao ya furaha.
Kumbuka ukigombana na huyo leo kisha ukamuacha na kuhamia kwa mwingine, mfumo wako wa kimapenzi utakuwa wa mashaka na unaweza kuonekana hujatulia kwani utakuwa ukiwabadilisha kila mara kwa kuwa tu huwa unagombana na hujui nini ufanye kumaliza mzozo.

1 comment: