Tuesday, October 07, 2014

Wiki mbili kabla ya kukutana na Yanga – Okwi apata majeruhi, Daktari azungumza

Zikiwa zimebaki takribani mbili kabla ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga, daktari wa Simba SC, Yassin Gembe amesema kwamba mshambuliaji, Mganda Emmanuel Okwi aligongwa kwenye enka na goti katika mchezo dhidi ya Stand United, lakini yuko fiti kabisa kucheza Oktoba 18, dhidi ya Yanga SC. Okwi alitolewa nje mara mbili kupatiwa huduma ya kwanza na Dk Gembe, lakini mara zote alirejea uwanjani kuendelea na mchezo. Pigo la pili lilimfanya mchezaji huyo aendelee kucheza huku akichechemea, hali ambayo ilizua hofu labda amepata maumivu makubwa. “Ni kweli Okwi aligongwa mara mbili, mara moja kwenye enka na mara moja kwenye goti. Lakini hayakuwa maumivu makubwa na ataendelea na mazoezi na wenzake” amesema Gembe Aidha, Dk Gembe amesema kwamba kipa Ivo Mapunda na beki Nassor Masoud ‘Chollo’ wataanza mazoezi ya kujiweka fiti wiki hii. Ivo aliumia kidole na anatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, hivi sasa akiwa yupo katika wiki ya tatu, wakati Chollo aliyeumia mkono, anatakiwa kuwa nje kwa wiki tatu, hivi sasa akiwa anaingia katika wiki ya pili. “Hawa wachezaji maumivu yao hayawazuii kufanya mazoezi ya kujiweka fiti, kwa hivyo niliwapa mapumziko mafupi kabla ya kuanza mazoezi ya kukimbia na gym. Ivo nilimpa wiki mbili za kupumzika na Chollo wiki moja, kwa hivyo wote wiki hii wataanza mazoezi,” Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Haroun Chanongo ambao wiki iliyopita walifanya mazoezi mepesi, nao wataanza mazoezi kikamilifu na wenzao. Majeruhi mwingine wa muda mrefu Simba SC ni Mkenya, Paul Kiongera ambaye anatakiwa kuwa nje kwa wiki sita baada ya kuumia goti, hivi sasa akiwa katika wiki ya nne- na Dk Gembe amesema ‘fowadi’ huyo anaendelea vizuri.

0 comments:

Post a Comment