Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewasili jijini
The Hague, Uholanzi katika Mahakama Maalum
ya Kimataifa inayohusika na visa vya uhalifu
kwa viongozi wa nchi zilizoridhia mkataba huo,
ICC, kwa ajili ya kikao maalum kuhusu kesi
inayomkabili.
Siku ya Jumatatu, Rais Kenyatta alikabidhi
madaraka yake kwa muda kwa Naibu Rais,
William Ruto na kusisitiza kuwa anaondoka
nchini humo kama raia.
Akiwahutubia Wabunge mjini Nairobi, Kenyatta
aliwaambia kuwa yuko
tayari kuhudhuria kikao maalum alichotakiwa
kuhudhuria mjini Hague bila wasiwasi wowote.
Kenyatta alitakiwa na majaji wa mahakama hiyo
kufika ICC tarehe 8 mwezi huu kufafanua madai
a upande wa mashitaka uliodai kuwa serikali ya
Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo
hasa upande wa mashitaka kwa kukataa
kuipatia ushahidi unaohitajika katika kesi
inayomkabili kama vile rekodi zake za
mawasiliano ya simu na taarifa zake za kifedha.
Mbali na hilo, Ofisi ya kiongozi wa Mashtaka
Jumanne wiki hii imewaomba majaji wa
Mahakama hiyo kuamua kuwa Kenya
haishirikiani na Ofisi hiyo kuhusu kesi
inayomkabili rais Kenyatta.
Kenyatta anakabiliwa na kesi inayomtuhumu
kupanga, kuchochea na kufadhili machafuko na
ghasia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2007.
Rais Kenyatta anasema anajiamini na kwamba
anajua hana hatia katika tuhuma zinazomkabili.
Alisema Kenya ni nchi huru na kwamba
haitawahi kuwa chini ya mamlaka nyingine
yoyote.
Vyombo kadhaa vya habari na mitandao ya
kijamii imeripoti kuwa takriban wabunge mia
moja walikuwa wanajiandaa kuambatana na
Kenyatta kuelekea The Hague katika ishara yao
ya kumuunga mkono.
0 comments:
Post a Comment