Tuesday, October 21, 2014
 |
KOCHA wa Simba, Patrick Phiri,
amepanga kufumua kikosi chake katika
usajili wa dirisha dogo hapo Desemba
ambapo ametamka kuwa anahitaji kuwa
na makipa wanne wenye ushindani
mkubwa na kusisitiza ni lazima afanye
uamuzi mgumu juu ya hilo huku akitaka
uongozi umnunulie kipa wa Yanga, Juma
Kaseja.
Kwa sasa Simba ina makipa watatu; Ivo
Mapunda, Hussein Sharif ‘Casillas’ na
Manyika Peter ambaye usajili wake ni
wa U-20.
Hiyo inamaanisha kwamba Kaseja
akitua Simba uwezekano wa Mapunda
kurejea Ligi Kuu Kenya ni mkubwa
kama ilivyoanza kuvumishwa kwani
Simba itakuwa na makipa wanne na
nafasi yake kucheza itakuwa finyu. Phiri
ameliambia Mwanaspoti kuwa alipatwa
na wakati mgumu baada ya makipa
wake wawili kuumia Ivo na Casillas na
kubakiwa na mmoja tu Manyika ambaye
hata hivyo alionyesha kiwango cha juu
katika mechi yao na Yanga iliyochezwa
Jumamosi iliyopita na kutoka suluhu.
Baada ya mechi hiyo, Phiri alisema
kuwa Manyika ana kiwango kikubwa
lakini anahitaji awepo na kipa mbadala
huku akitamani kumnasa Kaseja ambaye
aliwahi kuidakia Simba kwa miaka 10.
“Binafsi huwa namkubali Kaseja kuwa
ni kipa bora kutokana na uwezo wake
wa kudaka, ningependa kuwa naye
kwani nimewahi kumfundisha na
ninajua uwezo wake, nina makipa
watatu ambao ni wazuri lakini kuelekea
mechi ya Yanga wawili walikuwa na
majeruhi, nilikuwa katika wakati
mgumu ingawa nilimwamini Manyika,”
Phiri alisema.
“Nikisajili kipa mzoefu itanibidi niwe na
uamuzi mgumu katika upangaji kwani
ni lazima nikimtumia Manyika kutokana
na uwezo aliokuwa nao, nikimkalisha
benchi nitaua kiwango chake,
atakuwepo kipa namba moja lakini wote
watadaka kulingana na mechi zilivyo.”
Kaseja kwa sasa hapati nafasi ya kudaka
katika kikosi cha Yanga kwani kocha
Marcio Maximo amemwamini kipa Deo
Munishi ‘Dida’.
Kuhusu safu ya ulinzi, Phiri alisema:
“Pale kati Joseph Owino na Hassan
Isihaka wanatosha sina haja ya kusajili,
lakini beki wa pembeni ndio kuna tatizo
kwani wapinzani wetu wamegundua
tatizo hilo, hivyo nitaimarisha pembeni,
kiungo mkabaji ambapo kwa sasa
namtegemea sana Jonas Mkude.
Nitaongeza na straika mmoja.”
Kwa hesabu za Phiri basi uongozi wa
Simba ambao msimu huu umesajili
wachezaji 29 na kubakiwa na nafasi
moja ili wafike 30 watalazimika
kupunguza baadhi ya wachezaji wao ili
wasajili wachezaji ambao kocha
atapendekeza katika nafasi husika.
Phiri aliongeza: “Matokeo haya
(mfululizo wa sare) sio mazuri kabisa
kwetu, tunahitaji ushindi, lakini pia ni
bora tumetoka sare na Yanga kuliko
wangetufunga maana ingeleta shida
zaidi, tunaenda kucheza na Prisons
ambao sijawaona uwezo wao hivyo
lazima niongeze mbinu za kiufundi
kuhakikisha ushindi ugenini
unapatikana.”
Simba ilianza mazoezi yake jana
Jumatatu jioni, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. |
0 comments:
Post a Comment