Friday, September 26, 2014
 |
Na Dina Ismail, DAR ES SALAAM
MECHI ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga
SC mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara iliyokuwa ichezwe
Oktoba 12, mwaka huu imefutwa na sasa tarehe
mpya itatajwa kesho.
Taarifa ya TFF leo imesema kwamba, hiyo
iantokana na mchezo wa kirafiki wa kimataifa
baina ya Taifa Stars na Benin ambao kwa
ujumla utabadilisha ratiba ya Ligi Kuu na
marekebisho hayo yatatangazwa kesho
(Septemba 26 mwaka huu).
Taifa Stars inashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka
huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya
kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa
(FIFA).
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo
itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaendelea na
taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo
usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo
inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10
mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na
mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa
dini ya Kikristo na Kiislamu.
Wakati huo huo: Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi anatarajia
kufunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa
vyama vya mpira wa miguu wa wanawake vya
mikoa ya Tanzania Bara.
Hafla ya kufunga mafunzo hayo itafanyika kesho
(Septemba 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi
kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam.
Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha
viongozi 34 wakiwemo baadhi ya waandishi wa
habari na Meneja wa Twiga Stars, na
yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry
Tandau. |
0 comments:
Post a Comment