Thursday, September 04, 2014
 |
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
BAO pekee la Mbrazil Genilson Santana Santos
‘Jaja’ limeipa Yanga SC ushindi wa 1-0 katika
mchezo wa kirafiki dhidi ya Thika United ya
Kenya katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jaja alifunga dakika ya 58 kwa pasi ya Simon
Msuva na hilo linakuwa bao la pili kwa Jaja
tangu ajiunge na Yanga SC miezi miwili
iliyopita, akiwa amecheza mechi yake ya nne
leo.
Jaja aliingia ‘mzima mzima’ pembezoni mwa
lango la Thika kuhakikisha anaiunganishia
nyavuni krosi ya Msuva kwa vyovyote na
akafanikiwa akimuacha kipa Mganda, Hamza
Muwonge anaokota mpira nyavuni.
Kwa furaha ya bao hilo, Jaja ambaye alikuwa
akizomewa na mashabiki wa Simba SC kila
alipokosea alitoka nje ya Uwanja kushangilia
bao hilo, kwa shangwe za aina zote alizoweza.
Yanga SC haikucheza vizuri kipindi cha kwanza
na zaidi ilitegemea kupitisha mashambulizi
yake pembeni walipokuwa wakiteleza kwa
awamu Simon Msuva, Haruna Niyonzima na
Andrey Coutinho.
Coutinho alikaribia kufunga mara mbili kwa
mipira ya adhabu aliyopiga kutoka nje kidogo
ya eneo la penalti, wakati Jaja hakuwa na
madhara kabisa kipindi cha kwanza.
Nafasi nzuri zaidi kwa Thika ilikuwa dakika ya
20 wakati shuti la Moses Odhiambo
lilipodakwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’- zaidi
ya hapo, safu ya ulinzi ya Yanga SC leo ilicheza
vizuri.
Kipindi cha pili, kocha Mbrazil Marcio Maximo
alianza na mabadiliko katika safu ya kiungo
akimpumzisha Hassan Dilunga na kumuingiza
Hamisi Thabit, ambaye alikwenda kuibadilisha
timu.
Angalau Yanga wakaanza kucheza mpira, pasi
zilionekana kutembea uwanjani na mashabiki
wakaanza kushangilia ‘chama lao’.
Ni Hamisi Thabit ambaye alimpasia mpira
mzuri Msuva, aliyemtoka beki wa Thika hadi
nje kidogo ya eneo la penalti alipomtilia krosi
Jaja, aliyefunga bao hilo pekee.
Refa Hashim Abdallah aligoma kutoa penalti
dakika ya 62 baada Coutinho kuangushwa
kwenye eneo la hatari, wakati Said Bahanuzi
aliyetokea benchi alichelewa kuunganisha
krosi nzuri ya Niyonzima dakika ya 80.
Huo unakuwa mchezo wa nne kwa Maximo
tangu aanze kazi Yanga SC Julai mwaka huu na
amefanikiwa kushinda mechi zote, 1-0 dhidi
ya Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba kabla
ya kushinda 2-0 mara mbili dhidi ya Shangani
na KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi
‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu
Twite, Hassan Dilunga/Hamisi Thabit dk46,
Haruna Niyonzima/Omega Seme dk73,
Genilson Santana ‘Jaja’/Said Bahanuzi dk87,
Andery Coutinho/Nizar Khalfan dk60 na Simon
Msuva/Hussein Javu dk70. |
KAMA BADO UJAJIUNGA NASI BOFYA HAPA ILI KILA NIKIPATA HABARI ZIKUFIKIE KIRAHISI PUNDE NIZIPATAPO
Posted via Blogaway
0 comments:
Post a Comment