Saturday, September 27, 2014
 |
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
MECHI ya watani wa jadi, Simba SC na
Yanga SC mzunguko wa kwanza wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itapigwa
Oktoba 18, mwaka huu Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam badala ya Oktoba 12.
Mechi zote za Oktoba 11 na 12
zimesogezwa mbele kwa wiki moja kupisha
mchezo wa kimataifa, kati ya Tanzania na
Benin.
Taifa Stars itashuka uwanjani Oktoba 12
mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya
kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA).
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya
mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha
Mkuu Mart Nooij.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya
mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja
nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa
na msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na
mechi ya kudumisha upendo kati ya
viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Na kwa sababu, TFF imesogeza mbele
mechi zilizokuwa zichezwe wikiendi ya
Oktoba 11 na 12 na sasa zitachezwa Oktoba
18 na 19.
Oktoba 18, Polisi Morogoro itamenyana na
Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro, Ndanda na Ruvu Shooting
Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara,
Kagera Sugar na Stand United Uwanja wa
Kaitaba, Bukoba, Coastal Union na Mgambo
JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya
City na Azam FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya
na Yanga na Simba Taifa.
Mzunguko huo utahitimishwa na mchezo
kati ya Prisons na JKT Ruvu Uwanja wa
Sokoine, Mbeya Oktoba 19.
Zaidi ya hapo, Ratiba ya Ligi Kuu inabaki
kama ambayo ilitolewa awali na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF). |
0 comments:
Post a Comment