Tuesday, August 26, 2014

SASA SIMBA WAIKEJELI VIBAYA SANA YANGA

VIONGOZI wa Simba wameiangalia Yanga katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Shangani na wakatamka kauli ambazo ni kama wameipuuza kwa kusema: “Yanga wenyewe ndiyo hawa? Watatukoma.” Lakini kejeli hiyo ya Simba imekuja siku moja baada ya Kocha Marcio Maximo kutamka kwamba yupo makini na kila anachofanya na hawezi kuonyesha makucha yake hapa Unguja kwa vile anajua anafuatiliwa. Hivyo licha ya kwamba wanashinda lakini kocha huyo alisisitiza kwamba kinachoonekana sasa ni utangulizi ‘trela’ tu picha lenyewe bado. Vigogo wa Simba walioishuhudia Yanga yenye mastraika wawili Wabrazili ni Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kassim Dewji, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collins Frisch, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Mohamed Nassoro na Makamu wake, Idd Kajuna, wajumbe wengine ni Adam Mgoyi, Mohamed Omary na Hussein Simba. Mbali na hao, kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye pia aliwaona wachezaji wote wa Yanga kwenye mchezo huo akasema Maximo ana kazi ya ziada kurekebisha kikosi chake kwani kina upungufu. “Nimeona mechi lakini bado kuna mapungufu, Maximo anatakiwa kufanya kazi ili kuimarisha kikosi chake,” alisema Phiri huku akiishudia Yanga ikishinda mabao 2-0. “Kazi wanayo, kwa soka lile Maximo anatakiwa kufanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha kikosi hakimsumbui msimu ujao, wamecheza chini ya kiwango tofauti na tulivyofikiria,” alisema. Kwa upande wa Dewji yeye alisema: “Kikosi chetu kimecheza vizuri sana (dhidi ya Kilimani City) japokuwa kina udhaifu mdogo ambao kocha atarekebisha, lakini nimeangalia mechi ya Yanga haijanifurahisha, wana kazi. “Kilimani City ni wazuri na wamecheza soka safi ambalo kila mmoja aliyefika kuangalia amefurahia, hata sisi wenyewe tumekubali kuwa timu hiyo ni nzuri ingawa sisi ni wazuri zaidi.” Katika mechi ya Simba ambayo ilikuwa ya kirafiki kama ile ya Yanga na Shangani, Simba ilishinda bao 2-1. Mabao ya Simba yalifungwa na Shaban Kisiga kwa njia ya penalti na jingine lilifungwa na Haruna Chanongo.credit mwanaspoti

 BONYEZA HAPA KUSOMA HABARI NYINGINE 

0 comments:

Post a Comment