Tuesday, August 26, 2014

Emmanuel Okwi sasa akutana na kiboko yake

KAMA Emmanuel Okwi alizoea kudekezwa na viongozi wa Yanga, sasa amekutana na kiboko yake jambo ambalo huenda likamshtua yeye sambamba na wachezaji wengine wa kigeni. Kocha pekee mkuu Mbrazil kwenye Ligi ya Tanzania, Marcio Maximo ametamka kuwa anawajua wachezaji watano tu wa kigeni Yanga na ndio atakaowatumia. Miongoni mwao jina la Okwi ambaye yupo Dar es Salaam halimo. Maximo amesema atafanya kazi na Hamis Kiiza raia wa Uganda, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite pamoja Wabrazili Andrey Coutinho na Genilson Santos ‘Jaja’ ndiyo anaowatambua. Pamoja na wachezaji hao watano wanaofanya mazoezi ya pamoja, Yanga ina mkataba na Okwi anayefanya timu kuwa na wachezaji sita wa kigeni idadi ambayo hadi kesho Jumatano siku ya kufunga dirisha la usajili lazima ipunguzwe kwa mmoja kukatwa. Akizungumza na Mwanaspoti, Maximo alisema: “Ninao wachezaji watano tayari wa kutoka nje ya nchi kwenye timu yangu, hao ndiyo nitakaofanya nao kazi msimu huu. “Huyo Okwi sijamwona na hajaripoti kwenye timu yangu nifanyaje? Nitafanya kazi na hao tu.” Awali Kiiza ndiyo alikuwa aachwe, lakini sasa hali imeanza kuwa shwari kwake kutokana na nidhamu yake na jinsi anavyojituma mazoezini. Okwi ambaye alikuwa anapewa kipaumbele lakini alichelewa kujiunga na timu kwa sababu zisizojulikana, inadaiwa kuwa uongozi umemwambia ajieleze kwa barua na baada ya hapo atapewa adhabu ambayo ni siri. Kocha Msaidizi wa Yanga, Leonardo Neiva ambaye pia ni Mbrazili, alisema wamefurahishwa na uwezo wa straika Kiiza na kukiri kuwa ana sababu zote za kubaki Yanga. Aliliambia Mwanaspoti kuwa wamependa vigezo vitatu alivyonavyo straika huyo ambavyo ni nguvu, mipango mizuri ya uwanjani na uwezo wake wa kucheza kwenye nafasi tatu tofauti kwa ufasaha. “Anaweza kucheza kiungo vizuri tu kwani ana nguvu, kasi na vilevile mbinu , ana uwezo mkubwa wa kucheza winga na anatoa krosi nzuri na zenye malengo huku akikimbia kwa kasi, anacheza nafasi ya straika wa mwisho pia,” alisema Neiva.Source mwanaspoti

 >>>>>>>>> BOFYA HAPA <<<<>>>uhungane nasi

0 comments:

Post a Comment