Monday, August 25, 2014

Maximo aizuga vibaya timu ya Simba

YANGA walikuwa kambini mjini Pemba lakini juzi Jumamosi wakatua Unguja na jana Jumapili wakakipiga na Shanghani mchana kwenye mechi ya kirafiki katika Uwanja wa Amani. Ujio wa Yanga Unguja kiufundi ni faida pia kwa Simba ambayo imeweka kambi yake eneo la Mbweni ikifanya mazoezi Uwanja wa Chuoni. Yanga itapata nafasi ya kuisoma Simba kwenye mechi zake za kirafiki mpaka mazoezini na Simba nao hivyohivyo. Lakini Kocha Marcio Maximo ameshitukia hali hiyo na kutamka kwamba anafanya mambo yake kwa akili sana na hakuna timu yoyote itaweza kusoma mbinu zake kwani hatazitumia hadharani kwa muda wote atakaokuwa Unguja. Kocha huyo ambaye timu yake ina wachezaji wawili raia wa Brazil, alisema kwamba anafanya mambo kwa umakini sana na hata mbinu zake za maangamizi atawapa wachezaji katika mazingira ya siri. Anamaanisha kwamba hata Simba au Azam wakiangalia mechi yake yoyote ya kirafiki kwa sasa haitawasaidia. “Unajua tunakwenda kwenye ushindani kucheza ligi, kila mtu anataka kujua una mbinu gani hivyo suala hilo niko makini nalo sana, sitaki watu wagundue mbinu zangu, ”alisema Maximo ambaye bado hajatangaza kumuacha mchezaji wake ghali wa kigeni, Mganda Emmanuel Okwi licha ya kuchelewa. Keshokutwa Jumatano, Yanga itacheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Shangani na baada ya hapo, watarudi Dar es Salaam kucheza mechi mbili ngumu. Yanga awali ilicheza na Chipukizi na Shanghani. Katika hatua nyingine, Mbrazili Andrey Coutinho amewavutia zaidi mashabiki wa Pemba. Kocha Mkuu wa Chipukizi ya Pemba iliyofungwa na Yanga bao 1-0, amesema yeye ni Coutinho tu kwenye kikosi hicho na kilichomvutia zaidi ni namna anavyotumia akili kupenya sehemu ngumu. Coutinho anachezesha timu vizuri, pasi zake zenye macho zilimfanya Mbrazili mwenzake, Genilson Santos Santana ‘Jaja’ ang’ae kwenye mechi yao na Chipukizi ya Pemba. Mchezaji huyo mwenye mwili mdogo, ana kasi na alishirikiana vizuri na Mrisho Ngassa, Mnyarwanda Haruna Niyonzima katika kuchezesha timu. Kwenye Uwanja wa Gombani, kila alipokuwa akiunasa mpira zilisikika kelele za mashabiki zikimshangilia. Credit mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment