Tuesday, October 07, 2014

HIKI NDICHO WAZIRI ALICHOWAAGIZA TFF KUKIFANYA KUHUSU 5% YA FEDHA ZA WADHAMINI WA KLABU

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, leo amekutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ule wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na kuagiza kusitishwa kwa zoezi la ukatwaji wa asilimia 5. TFF iliiagiza bodi kukata asilimia 5 ya fedha za klabu kutokana na udhamini wa Vodacom na Azam TV, halafu ziwekwe kwenye akaunti yake ili zitumike kwa maendeleo ya soka. Lakini katika mkutano wa leo, Nkamia amewasisitiza TFF, Bodi ya ligi na klabu kukutana, halafu kulijadili hilo suala. TFF wametakiwa kukutana kwa pamoja na wadau hao, halafu wafikie mwafaka kabla ya kurejea serikalini. “Wanatakiwa wakutane, wazungumze na kukubaliana na siku nzuri ya kufanya hivyo nimeona ni Jumamosi. “Baada ya hapo watakachofikia mwafaka, basi watarudi serikalini na sisi tuangalie, lakini suala la kukata fedha hizo kweli nimesitisha na sasa liangaliwe hilo la kukutana kwanza,” alisema Nkamia ambaye kitaaluma ni mwanahabari. Mkutano huo unasubiriwa kwa hamu kwa kuwa pande zote tatu zimekuwa na msimamo wa aina mbili. Bodi ya ligi pamoja na klabu hizo za ligi kuu, zimesisitiza haziwezi kukubaliana na hilo la kukatwa fedha zao za udhamini kwa kuwa mikataba ya Vodacom na Azam Tv iko wazi na haielezi hilo la asilimia tano. Lakini tayari TFF kupitia Rais wake Jamal Malinzi ilishatangaza suala hilo halitakuwa na mjadala na lazima wakatwe. Pia kwa hesabu za kawaida, inaonyesha TFF inachukua fedha nyingi zaidi kuliko hata klabu moja moja kupitia udhamini wa Vodacom na Azam TV.

 HABARI ZINGINE BOFYA HAPA 

0 comments:

Post a Comment