Sunday, August 31, 2014

Manji jeuri, aapa Okwi hachezi Simba

SIMBA kila kona nchini wanashangilia baada ya kumsainisha straika machachari mwenye mkataba na Yanga, Emmanuel Okwi. Lakini Mwenyekiti wa Yanga,Yusuf Manji, ameibuka na kutoa msimamo mkali kwa kusisitiza kwamba mchezaji huyo hatacheza Msimbazi. Manji aliyeonekana na uso wa furaha wakati wote wa mkutano wake na waandishi wa habari akiambatana na Makamu wake Clement Sanga, alisisitiza kwamba Yanga haiwezi kuwa chini ya mchezaji mmoja na kwamba hawajawahi kumuacha Okwi. Alisema kwamba wamemfungulia mashtaka ya kinidhamu TFF na hata katika orodha yao ya wachezaji wa kigeni waliopelekwa TFF jina la Okwi limo wakisubiri hatma ya kesi waliyoifungua. “Siku zote tumekuwa tukiwaheshimu hawa jamaa zetu, mtamkumbuka mara kadhaa nimekuwa nikiwapongeza hata wanapoifunga timu yangu, tumekuwa tukiwasajili wachezaji wengi wa Simba kama Kaseja (Juma), Yondani (Kelvin) lakini hatukuwa tunawasajili wakati wana mikataba tunasubiri mpaka mikataba yao inapomalizika,”alisema Manji. “Yanga hatuna desturi ya kulalamika waliondoka Kavumbagu (Didier) na Domayo (Frank) kwenda Azam hatukulalamika kwa kuwa utaratibu ulifuatwa na hata hili hatulalamiki kwa kuwa tunajua tunachokifanya, Yanga hatujamuacha Okwi, ni mchezaji wetu. “Inashangaza sana inawezekanaje mtu akawa na ugomvi na mkewe wakati huohuo kuna mtu mwingine anajitokeza kusikojulikana na kutangaza kufunga ndoa halali na mkeo, unaweza kujiuliza hawa watu wamekutana na kupatana wakati gani, linatutia shaka hili.” Manji alisema kwa kuwa tayari wameshafungua kesi ya kwanza ambayo kabla ya kujibiwa mchezaji husika ameongeza kosa lingine, sasa Yanga imewasilisha TFF mashtaka mengine ambayo sasa itawajumuisha Okwi, Simba na wakala wa mchezaji. Katika kesi hiyo sasa pande hizo tatu zitatakiwa kuilipa Yanga kiasi cha Dola 500,000 (Sh825mil). “Nina uwezo wa kuwanunua wachezaji wote wa Simba pamoja na kocha wao Phiri (Patrick) na kuwazuia wasicheze ligi wakae pale Gymkhana wachezee mpira na kulala, lakini nikifanya hivyo watu watalalamika Manji anaharibu mpira. “Najua kwamba mishahara ya wachezaji wangu wa Yanga ya miezi miwili pale Simba inawalipa wachezaji wao wote mwaka mzima, tunataka kuona TFF inawafungia Okwi na Simba tunatoa siku saba kujua hatma ya hilo ikishindikana hapo tutaenda Fifa na CAS (mahakama ya michezo),”alisisitiza Manji. TFF yamtambua Okwi Yanga TFF kupitia kwa Katibu wake Mkuu, Celestine Mwesigwa, amethibitisha kwamba ofisi yake haina mamlaka ya kutoa kibali chochote maalum cha kumpeleka Okwi kuichezea Simba ambapo kwa sasa bado wanamtambua mchezaji huyo kuwa ni mali ya Yanga.credit mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment