Monday, August 04, 2014

HIVI NDIVYO STARS ILIVYOTUPWA NJE NA MSUMBIJI

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam, Shomari Kapombe alilia sana mara baada ya kumalizika kwa mchezo , na alijitolea kwa muda wote uwanjani , na ilikuwa hivyo pia kwa wachezaji wengine ambao hawakuamini matokeo ya kuondolewa kwa mara nyingine na Msumbiji na kufuta ndoto za Watanzania kuiona timu yao ikicheza fainali za Afrika baada ya miaka 34.

Mwalimu, Nooij alifanya mabadiliko katika nafasi ya ulinzi wa kushoto baada ya kumuacha nje Oscar Joshua ambaye alionyesha kuwa mzito katika mchezo wa kwanza na kumuinga mlinzi, Said Mourad. Stars ilicheza mfumo wa kujihami lakini kwa kutumia wachezaji wengi wenye kasi. Erasto Nyini alicheza kama kiungo wa ulinzi akisaidiwa na Mwinyi Kazimoto ambaye alicheza kama kiungo wa mashambulizi Msumbiji ilifanya mashambulizi mfululizo kiasi cha kufanya Stars ‘ kuelemewa’ na kupokea mashambulizi mengi.

Krosi kutoka upande wa kulia wa Stars ilimaliziwa vizuri na mchezaji, Josimar Macheisse katika dakika ya 45.

Hadi nusu ya kwanza inamalizika, Stars ilikuwa nyuma kwa bao 1-0. Nooij aliamua kuwaanzisha, Thomas Ulimwengu, Hamis Macha, Mbwana Samatta na John Bocco kwa lengo la kupata bao la mapema, lakini timu ikakosa ‘ balansi’ na wachezaji wa nafasi ya kiungo wakaonekana kuchoka mapema na kuanza kupoteza umakini. Amri Kiemba aliingia mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili kwa lengo la kuimarisha nafasi ya kiungo. Mcha ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, alishindwa kucheza vizuri katika wingi, kiasi cha kufanya upande wa kulia kuwa dhaifu.

Nooij alifanya maamuzi sahihi katika wakati sahihi kwa kumtoa Mcha na kumuingiza Kiemba lakini alifanya kosa namna ya kuwapanga wachezaji hao wanne. Hakukuwa na sababu ya kumuanzisha Bocco, kwa sababu haikuwa mechi ya kujaribu.

Stars ilifanya mashambulizi machache katika kipindi cha kwanza lakini yalikuwa na mipango iliyokamilika. Mourad alikaribia kufunga bao baada ya kuunganisha vizuri mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mcha lakini Batte aliokoa mpira huo uliokuwa ukielekea nyavuni mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Kabla ya kufungwa bao la kwanza mwamuzi wa pembeni alimnyoshea kibendera Bocco ambaye alikuwa ‘ on side’ kwa madai kwamba ameotea. Ilikuwa ni kitendo ambacho kiliwachanganya wachezaji na benchi la ufundi, huku kocha Nooij akionyesha kulalamika wazi. Ilikuwa ni dakika 44, dakika moja kabla ya Msumbiji kupata bao. UKitoa sababu za uchezeshaji mbaya wa waamuzi, Dennis Batten a wasaidizi wake, Stars ilizidiwa uwanjani kutokana na upangaji mbaya wa kikosi.

Kiemba alionekana kuinua timu na kufanya wachezaji kupiga pasi na kupanga mashambulizi Samatta alifunga bao la kusawazisha robo saa kabla ya kumalizika kwa mchezo huo baada ya kumkimbiza beki wa Msumbiji hadi karibu na lango na kupiga ‘ kiki kali’ iliyomshinda mlinda mlango wa Msumbiji, Dario Khan Elias Pelembe ‘ Domingues’ alifunga kwa mkwaju wa penalti katika mchezo wa sare ya mabao 2-2 wiki mbili zilizopita. Mchezaji huyo wa klabu ya Kaizer Chiefs alitulia na kupiga kiufundi mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja nyavuni na kumshinda kipa Deogratius Munishi baada ya kuangushwa na Kelvin Yondan nje kidogo ya eneo la hatari.

Bao hilo la dakika ya 81 lilimaliza kasi ya Stars ambao walishambulia mfululizo mara baada ya kupata bao la kusawazisha. SARE YA MABAO 2-2, DAR ES SALAAM. Kitendo cha kukubali bao la kusawazisha zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita ilikuwa ni matokeo nafuu kwa wageni. Msumbiji ilicheza mchezo wa taratibu ugenini huku wakipanga mashambulizi ya uhakika na kufanikiwa kufunga mabao mawili ambayo yaliwaweka katika hali ya kujiamini kuelekea mchezo wa marejeano.

Kitendo cha kufunga mabao mawili ya ugenini ambayo kufutwa kwake ilibidi Stars kufunga mabao mawili, jijini, Maputo jambo ambalo halikuwezekana.

SAFU YA ULINZI. Shomari Kapombe alionyesha kutojiamini katika mchezo wa kwanza, na ni hivyo pia ilivyokuwa katika mchezo wa kipigo cha mabao 2-1 siku ya Jumapili.

Mchezaji huyu si mzuri akicheza kama mlinzi wa kulia, si mkabaji mzuri na hawezi kucheza katika maeneo yake kama mlinzi wa pembeni wakati timu ikishambuliwa. Ni kweli hakuna namba mbili wa asili kutoka katika klabu 14 za ligi kuu? Kama safu ya walinzi wa pembeni si imara ni lazima safu ya kati itayumba.

Kitendo cha kufungwa mabao nane katika michezo mitatu ni kielelezo tosha kuwa safu ya ulinzi ni dhaifu, na ili kuiimarisha zaidi ni lazima wachezaji wachaguliwe kutokana na namba wanazocheza na si wachezaji viraka, Mourad alianza mahali kwa Oscar.

Kelvin Yondan ameendelea kufanya makosa yaleyale. PASI MKAA. Kupiga pasi ni tatizo kubwa kwa wachezaji wa Tanzania. Kama mchezaji hutokimbia uwanjani timu haiwezi kucheza pasi zinazofika. Kuanzia katika ligi kuu hadi michuano ya kimataifa wachezaji wengi wa Kitanzania wanapiga pasi ‘ laini’ zisizo na nguvu kiasi cha kufanya wachezaji kucheza kwa spidi ya chini.

Msumbiji walikuwa wakipigiana pasi za nguvu ambazo nyingi zilifika kwa walengwa tofauti na wachezaji wa Stars ambao walipiga pasi nyingi zisizo na nguvu. Tanzania ni moja ya nchi zinazosotea kufuzu kwa fainali za Afrika kwa miongo mitatu sasa na safari zote zimekuwa na mwisho wa kukatisha tamaa.

Stars imefanikiwa kunolewa na kocha Martin Nooij ambaye ana uzoefu wa kutosha katika soka la barani Afrika. Nooij aliifundisha Msumbiji kwa miaka miwili na aliisaidia timu hiyo kufuzu kwa fainali za Afrika, mwaka, 2010, nchini, Angola. Ni kocha mwenye tamaa ya mafanikio. Nafasi ya mshambuliaji, Mbwana Samatta imekuwa tatizo. Timu pinzani zinaingia uwanjani kwa ajili ya kumuangalia yeye tu. Bao la kusawazisha katika dakika ya 78 limefikisha ujumbe kuwa mchezaji ataisaidia sana Stars kama atapangwa katika nafasi ya mshambulizi wa kwanza.

Vipaji vingine kama, Thomas Ulimwengu, Hamis Mcha, na wengineo vinaweza kutumika katika nafasi nyingine za ushambuliaji. Ukuta mzuri ndiyo mbinu sahihi ya kushinda mechi. Kutupwa nje kwa Stars ni kutokana na udhaifu katika ngome. Katika michezo minne iliyopita safu ya mashambulizi imefanikiwa kufunga mabao saba, huku mabao matano yakifungwa ugenini ni kigezo sahihi ya maendeleo katika nafasi ya ufungaji. Kumpanga, Samatta kama mshambuliaji wa pili kumechangia kuondoshwa kwa Stars.

Kama bado ujaungana nasi ili kila tukipata habari zikufikie kirahisi BONYEZA HAPA 

0 comments:

Post a Comment