KOCHA wa Yanga, Mbrazili Marcio Maximo amesema anaweza kutumia fomesheni tatu katika mechi moja kutokana na uzito wa mechi husika. Maximo ambaye anapendelea kutumia mifumo ya 4-4-2, 4-2-3-1, 4-3-3 na 4-5-1 alisema uzito wa mechi iliyoko mbele yake unaweza kumlazimisha kubadili mifumo kadhaa ndani ya mechi moja ili kuhakikisha kuwa anapata matokeo mazuri.
“Mpira wa sasa ni tofauti na kipindi nilipokuwa nacheza mimi miaka 25 iliyopita, kipindi hicho kocha alikuwa akitumia mfumo mmoja pekee katika mechina tulilazimika kuutumia huo huo kupata ushindi.
“Kwa sasa mambo yamebadilika, naweza kutumia mifumo miwili, mitatu au zaidi katika mechi moja ili kupata matokeo mazuri. Huo ndiyo mpira wa kisasa na ndiyo ninaotarajia kuutumia Yanga,” alisema Maximo na kuongeza “Sitaki timu yangu iweze kutabirika, nitatumia aina mbalimbali za uchezaji ili kuhakikisha wapinzani hawatambui ni ipi hasa itakuwa dhidi yao.
Nitajitahidi kuchanganya ya kupiga mipira mirefu kutokea kati kwenda kwa mawinga na pia kutumia mashambulizi ya mipira ya kupenyeza.” Wachezaji washindwa kumchezesha Jaja Katika mazoezi ya Yanga hapo jana wachezaji wa timu hiyo walishindwa kupiga mipira ya krosi zinazomfikia mshambuliaji wao Geilson Santos ‘Jaja’ na kumfanya straika huyo kucheza kwa kipindi chote cha mazoezi bila kufunga bao hata moja.
Mabeki wa pembeni Juma Abdul na Salum Telela waliokuwa wakipiga krosi hizo walikwama mara nyingi kupiga mipira ya juu inayomfikia Jaja kitendo kilichomweka straika huyo katika wakati mgumu. Maximo alisema ugumu wa uwanja wa Loyola wanaofanyia mazoezi ndiyo unaowafanya wachezaji hao kushindwa kupiga krosi za juu lakini anaendelea na jitihada za kuangalia namna sahihi ya kumtumia straika huyo.
“Uwanja ni mgumu sana, nimewaruhusu kupunguza hata kasi wanapopiga krosi ili wapige krosi nzuri lakini bado imekuwa tatizo, naendelea na jitihada kuona namna sahihi ya kulifanya hilo lakini natumai kwenye uwanja mzuri litakuwa linawezekana,” alisema Maximo.
Source mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment