KOCHA wa Simba, Zdravko Logarusic amesema kwamba moja ya sifa anazozitaka kwa mchezaji mpya atakayesajiliwa kwenye kikosi chake ni mchezaji mwenye utayari wa kucheza na kumtaja Paul Kiongera kuwa amekidhi sifa zote na ni straika kamili.
Kiongera ni mchezaji anayeichezea timu ya KCB ya Kenya na amewahi kufundishwa na Loga akiwa na timu ya Gor Mahia ambapo sasa yupo mbioni kusajiliwa na Wekundu hao wa Msimbazi. “Kiongera ni mchezaji aliyekamilika, anajua namna ya kufunga na kufanya uamuzi sahihi uwanjani, anasajiliwa ili acheze hivyo nitaangalia namna ya kumchezesha pamoja na Amissi Tambwe au ikiwezekana na mshambuliaji mwingine wa tatu,” alisema Loga.
Alisema hata alipopendekeza usajili wa beki Donald Mosoti ambaye pia aliichezea Gor Mahia, alijua wazi kuwa anakuja kucheza soka. “Ndiyo maana hata nilipohitaji Mosoti aje Simba nilijua kiwango chake na uwezo wake, hata Kiongera namfahamu vizuri ana sifa zote,” alisema .
Mshambuliaji huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa kuna uwezekano mkubwa akatua nchini kesho Jumapili ili kumalizana na viongozi wa Simba na yupo tayari kuitumikia klabu hiyo. Endapo watakubaliana, Simba watalazimika kuvunja mkataba na mchezaji huyo kwani amesaini mkataba wa miezi sita unaomalizika Novemba mwaka huu.
Source mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment