HATIMAYE Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, ametoa maelezo yenye kuwiana na mtazamo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwa pamoja katika nyakati tofauti, wakiashiria uwezekano wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka kundi maalumu linalojitambulisha kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea bungeni Agosti, mwaka huu.
Katika hali inayoashiria viongozi hao muhimu katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya wameanza kuzungumza “lugha” inayofanana, Sitta katika mazungumzo yake na mwandishi wetu alisema “kuna mambo mengi ya msingi ya kujadili kwa manufaa ya taifa si tu muundo wa idadi ya serikali”.
Kauli inayowiana kimantiki na Warioba aliyepata kumweleza mwandishi wetu kwamba; “Tumekubaliana kutoa wito, hasa kwa viongozi wa kitaifa, wa siasa na wa dola, washauriane kwa dhati kabisa chini ya maelewano ya kuhakikisha kwamba Katiba mpya inapatikana.
Ishara njema kwa kauli za viongozi hao inatiwa nguvu zaidi na aina ya watu walioshiriki mazungumzo baada ya mwaliko wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, ambaye aliweka bayana kwa mwandishi wetu kwamba walijikusanya wakiwa 20 katika Hoteli ya White Sands jijini Dare s Salaam mwezi uliopita, kujadiliana kuhusu kunusuru mchakato wa Katiba mpya, wakiwaalika baadhi ya wasomi na wajumbe wenye ushawishi ndani ya makundi yanayokinzana katika Bunge la Katiba.
Ingawa haijawekwa bayana na Jaji Warioba, lakini ni dhahiri kwamba mwaliko wa Profesa Abdul Sheriff, anayeaminika kuwa na ushawishi mkubwa katika kundi la UKAWA ambaye pia ni mjumbe wa Bunge la Katiba, pamoja na mwaliko wa Kingunge Ngombale Mwiru, mwenye ushawishi mkubwa katika kundi la Tanzania Kwanza, linalokutanisha wajumbe wengi wa Bunge la Katiba kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ni matukio yanayochagiza uwezekano wa UKAWA kurejea bungeni japo kwa masharti maalumu kwa wenzao, Tanzania Kwanza.
Profesa Sheriff ni msomaji anayeheshimika ndani na nje ya nchi, mwenye uwezo mkubwa wa kupima na kuchambua hoja mbalimbali za masuala ya kijamii na utawala na kwa hiyo, katika kikao chao na akina Jaji Warioba, alikuwa na mchango wa kipekee, alitoa hoja zake kwa mtazamo wake lakini zikiwa zimebeba ujumbe wa kunusuru mchakato wa Katiba mpya, kama ilivyo kwa mwenzake, Kingunge.
Maelezo ya Jaji Warioba Katika mazungumzo yake na gazeti la Raia Mwema ambayo vile vile yalichapishwa siku ya Jumanne katika gazeti dada na hili la Raia Tanzania, Warioba alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kitaifa, wa siasa na wa dola kushauriana kwa dhati ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya. Alitoa ushauri huo katika wakati ambao Bunge Maalumu la Katiba likitarajiwa kuanza tena vikao vyake mwezi ujao huku kukiwa na wasiwasi wa vikao hivyo kukwama kutokana na kundi kubwa la wajumbe wa upinzani, UKAWA, kuwa katika hatihati ya kushiriki.
Maoni hayo ya Tume ya Jaji Warioba ni matokeo ya kikao cha faragha cha baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo kilichofanyika wiki iliyopita kutafakari mustakabali wa mchakato wa Katiba mpya baada ya Tume kumaliza kazi yake na majadiliano kuanza kwenye Bunge Maalumu. “Sisi, pamoja na kwamba kazi yetu ilikwisha kumalizika, ni wadau wa jambo hili la Katiba mpya.
Kwa hiyo baadhi yetu, tupatao 20, tulikwenda retreat (mkutano wa faragha) na tukaomba baadhi ya wataalamu na wasomi kuja kutufanyia tathmini ya jinsi mchakato unavyokwenda.
“Tulialika watu mbalimbali wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Na tulikuwa na watu kama Kingunge Ngombale-Mwiru na Profesa Shariff,” alisema Jaji Joseph Warioba katika mazungumzo na Raia Mwema kuhusu faragha hiyo ya siku nne mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba changamoto wanayoiona wao ni kama Bunge Maalumu litaendelea na hata kama litaendelea, kama kutakuwa na uamuzi muhimu utakaofikiwa kufuatana na matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hasa kuhusu kura za theluthi mbili kwa kila upande wa Jamhuri ya Muuungano.
“Tumeona kuna changamoto kubwa. Hakuna hakika kama Bunge litaendelea kwa ukamilifu. Hata likiendelea hakuna hakika kama kutakuwa na maamuzi kwa mujibu wa sheria, hasa ya theluthi mbili kwa kila upande kwa kuwa lipo kundi limetoka nje na hivyo maamuzi hayatakuwa rahisi. “Tumekubaliana kutoa wito, hasa kwa viongozi wa kitaifa, wa siasa na wa dola, washauriane kwa dhati kabisa chini ya maelewano ya kuhakikisha kwamba Katiba mpya inapatikana.
“Tumeona pia kwamba hata katika eneo la muundo wa Muungano, kilichozungumzwa sana ni upungufu wa muundo wa serikali tatu si marekebisho gani yafanywe. “Kwa hiyo ndiyo maana tukasema makundi hayo ya viongozi yashauriane, mchakato uendelee na tujue kuwa ni wajibu wa Rais kuhakikisha kwamba mchakato unaendelea,” alisema Jaji Warioba.
Maelezo ya Sitta Naye Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, alimweleza mwandishi wetu kwamba kwa sehemu kubwa kilichotokea katika Bunge Maalumu la Katiba (UKAWA kususa) ni masuala ambayo yanahusu zaidi vyama vya siasa na utatuzi wake unategemea zaidi vyama hivyo, ingawa Bunge lina nafasi yake vile vile.
“Masuala haya kwa sehemu kubwa yako mikononi mwa vyama vya siasa. Unajua tatizo lolote la kisiasa linahitaji ufumbuzi wa kisiasa, kwa hiyo sisi (Bunge Maalumu la Katiba) hatuwezi kuingilia moja kwa moja masharti na taratibu za vyama vya siasa katika utatuzi wa masuala yanayowahusu kwa sehemu kubwa. “Tunafanya jitihada lakini jitihada zaidi zinapaswa kufanywa na wanasiasa kupitia vyama.
Na kwa kweli tunatumaini masuala haya yatapata ufumbuzi wa kisiasa. Mkutano wa Bunge la Katiba utaendelea na kimsingi, kuna hoja nyingi zinazohusu wananchi moja kwa moja na si tu idadi ya serikali katika muundo wa Muungano. Kuna mengi mazito ndani ya Rasimu ya Katiba, kwa mfano, kuna suala la mamlaka na nafasi ya Zanzibar, hoja ya 50 kwa 50 na hoja nyingine kadhaa muhimu, tuna matumaini makubwa mambo yanaweza kuwa mazuri,’ alisema Sitta.
Kauli ya Waziri Mkuu Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mizengo Pinda hivi karibuni alitoa wito kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliosusa vikao vya Bunge hilo kurejea ili mjadala wa Rasimu ya Katiba uendelee vema, akipendekeza kutumia utaratibu wa maridhiano uliowekwa kikanuni kutatua tofauti zilizopo ndani ya Bunge la Katiba.
Alitoa wito huo alipokuwa akizungumza katika hotuba ya kufunga Bunge la Bajeti, mwishoni mwa wiki iliyopita, mjini Dodoma, akitoa ujumbe uliofanana na ule wa Rais Jakaya Kikwete, mara kwa mara kwamba njia pekee ya kupata suluhu kwa mgogoro uliojitokeza Bunge la Katiba ni wajumbe wa Bunge hilo kutumia fursa ya kikanuni hasa Kamati ya Maridhiano ya chombo hicho, kumaliza mgogoro kati yao. Waziri Mkuu Pinda katika maelezo yake alisema; “Ninapenda kuwashauri wajumbe wenzangu ambao wameamua kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kutafakari uamuzi na matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba na wajibu wao kwa wananchi.
“Sisi wote tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi hii muhimu tuliyopewa kisheria ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Katiba mpya.
Kwa kuwa waheshimiwa wabunge wote wa Bunge hili ni sehemu ya wajumbe wa Bunge Maalumu, naomba nitumie fursa hii kutoa ujumbe mfupi kwa wajumbe wa Bunge Maalumu ambao naamini utaweza kuwafikia popote walipo. “Kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatoa masharti na mamlaka ya Bunge Maalumu kutunga kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli za Bunge Maalumu. “Ni kwa kupitia mamlaka kama ilivyofafanuliwa katika kifungu hiki, wajumbe wa Bunge Maalumu waliweza kutunga Kanuni za Bunge Maalumu kwa maridhiano kwa muda wa takriban mwezi mmoja. Vile vile, ni kupitia kanuni hizo, viongozi wa Bunge Maalumu waliweza kuchaguliwa na kufanya Bunge hilo kuwa chombo maalumu chenye uongozi na kuwa na mamlaka yake ya kisheria “Kanuni ya 46 ya Bunge Maalum la Katiba inaeleza mambo yasiyoruhusiwa kwenye Bunge Maalumu, aidha, Kanuni hii ya 46 inatoa utaratibu mzima wa jinsi ya kushughulikia masuala haya ndani ya Bunge Maalumu. Kanuni ya 16 (3) inatoa nafasi kwa mjumbe au wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mwenyekiti uliotolewa, kuwa atakuwa na haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko yake kwa Katibu ndani ya siku moja kuanzia tarehe ya uamuzi.
“Kwa mwendelezo huo huo, Kanuni ya 59 (1) (d) inaelekeza kuwa, moja ya majukumu ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu ni kuchunguza kuhusu masuala yote ya haki, kinga na madaraka ya Bunge Maalumu yatakayopelekwa kwenye Kamati hiyo na Katibu kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge Maalumu. “Kutokana na utaratibu huo wa Kikanuni kama ilivyoainishwa katika Kanuni hizo za Bunge Maalumu, ninapenda kutumia fursa hii kuwashauri “wana UKAWA” ambao wengi wao wamo ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wenzangu wote wa Bunge Maalumu ambao wamo ndani na nje ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wetu kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge Maalumu kupeleka malalamiko yote katika Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalumu ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya Bunge Maalumu na siyo nje ya Bunge”. BONYEZA HAPA
festo saimon 0657035125
0 comments:
Post a Comment