Thursday, July 10, 2014

BILA UKAWA HAKUNA KATIBA

Wakati kukiwa na juhudi za watendaji wa Bunge maalumu la Katiba kuwashawishi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wawaruhusu wabunge wao kurejea bungeni wakati vikao vya Bunge hilo vitakavyoanza Agosti 5 mwaka huu, bado utata umegubika kuhusu uwezekano wa kupatikana katiba hiyo kwa wakati Hata hivyo tayari Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa kama katiba hiyo haitapatikana sasa, Katiba ya Muungano mwaka 1977, itaendelea kutumika.

Kwa wakati, siku na mara kadhaa zimefanyika juhudi hizo bila ya kuzaa matunda, huku viongozi wa vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, wakionekana kuweka ngumu na kutoa masharti kwa Serikali kama itataka warejee bungeni.

Ni dhahiri sasa msimamo huo umeendelea kuliweka taifa katika wakati mgumu hasa inapoonekana kuwa matumaini ya kupata Katiba Mpya yanaendelea kufutika.

Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba Yahya Khamis Hamad anatoboa siri ya Bunge kuchukua juhudi hizo na kusema hata hivyo bado hazijazaa matunda na hadi sasa bado haijafahamika kama wabunge wa kundi a Ukawa watarajea au la.

Hamad anazitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa hadi sasa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samuel John Sitta kukutana na viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti, akiwamo Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad mwenye ushawishi mkubwa kwenye kundi la Ukawa.

Aidha, chama cha CUF ndicho chama chenye Wawakilishi wengi katika Bunge la Katiba baada ya kuwa na wabunge wa kuchaguliwa, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wa kuteuliwa.

Akiwa Zanzibar, Sitta pia amekutana na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein chini ya agenda hiyo akihimiza na kuwataka wajumbe hao kurejea na kuhitimisha ng’we iliyobaki. Katibu wa Bunge la Katiba Mpya anabainisha kuwa matayarisho ya Mkutano wa Pili wa Bunge maalumu la Katiba yameanza kufanyika na kikao cha kwanza kinatarajiwa kuanza Agosti 5 mwaka huu, huku wakiwa na matumaini kuwa kundi la Ukawa litarejea na kushiriki vikao vya Bunge hilo.

Hamad anasema milango iko wazi kwa wabunge hao kurejea na kushiriki Bunge hilo ili kusaka suluhu kupitia kamati ya uongozi pamoja na ile ya maridhiano na kufikia mwafaka wa mvutano uliojitokeza badala ya kundi hilo kubaki nje ya Bunge.

Katibu huyo anaeleza kuwa haamini kama kuendelea kwa Ukawa kubaki nje ya Bunge ni njia sahihi na ya uhakika, badala yake angetamani warudi bungeni ili madai hayo yakafanyiwe kazi.

Pia amesema hatua ya wabunge wengi wa makundi maalumu miongoni mwa 201 kuendelea kubakia kwenye Bunge, ni jambo linalotia faraja na matumaini kama njia inayoweza kurahisisha kupata theluthi mbili ya wabunge wa Bunge hilo.

Kama unataka upate taarifa zozote zinazotufikia kwa haraka zaidi  BONYEZA HAPA 


UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon

0 comments:

Post a Comment