BABA wa mwanafunzi aliyefanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita na kushika nafasi ya pili kitaifa masomo ya sayansi, Doris Noah amesema mtoto wake ana ndoto ya kuwa rubani lakini bado hakubaliani na maamuzi yake.
Akizungumza katika chumba cha habari cha gazeti hili jana, Noah Odiero ambaye ni Mshauri na Mlezi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, amesema binafsi amefurahishwa na matokeo ya mtoto wake.
Hata hivyo alisema alikuwa akimshauri kusomea masuala ya uhandisi wa migodi na petroli, lakini matokeo yametoka sasa hivi tutaona tuchague nini.(MM) “Tanzania bado sana kwa taaluma hii nchi yenyewe haina ndege anaweza tu kupoteza taaluma yake,” alisema.
Akijibu swali nini anadhani siri ya ushindi kwa mwanae alisema ni kujisomea na kupenda kusali. “Namshukuru Mungu nimefurahi kwa mwanangu kufanya vizuri, lakini mpaka sasa sijaongea na mwanangu kwani sasa yuko kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT Kanembo Kigoma walivyofika kule wamenyang’anywa simu, sikuongea naye kwa vile nilikuwa nimeongea na afande labda atakuwa amemuambia,” alisema.
Alisema Doris ni mtoto mpole hasa akiwa nyumbani kama akiwa hana shughuli atakuwa nyumbani amepumzika na mara nyingi anapenda kujisomea vitabu. Pia alisema anapenda sana kusali na kitu kingine anachoamini kumsaidia mwanawe kufanya vizuri ni kukubaliana na matakwa yake.
Alisema Doris alizaliwa Julai 29, mwaka 1995 katika hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam na alisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Segerea ambapo baadaye shule hiyo ikagawanywa na kuwa shule mbili za Segerea na Maendeleo. Alisema Doris alihamia Maendeleo akiwa darasa la tano na alimaliza darasa la saba ambapo alifaulu na kupangiwa kwenda shule ya wasichana ya Kisutu.
Alisema wakati akisoma shule ya msingi alikuwa akishika nafasi za juu lakini licha ya kufaulu kwenda Kisutu aliomba asipelekwe Kisutu kutokana na matatizo ya usafiri na shida ya kuamka asubuhi. Alisema aliamua kumtafutia mtoto wake shule ya bweni katika Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro kwenye shule ya Sekondari ya wasichana ya Kandoto ambapo alisoma kidato cha kwanza kuanzia mwaka 2008 hadi 2011.
Odiero alisema kwenye mtihani wa kidato cha nne alipata daraja la kwanza pointi nane na kuwa wanafunzi kumi bora kitaifa. Odiero mwenye watoto wanne, anasema mkewe ni Neema Kidela ambaye ni mwalimu katika shule ya Msingi Ipagala B, Dodoma
CHANZO:HABARILEO
Kama bado ujaungana na mimi ili kila nikipata habari zikufikie kilahisi
>>>>>>>>>BONYEZA HAPA >>><<
UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon
0 comments:
Post a Comment