Monday, October 20, 2014

MILIONI 58 ZAFUTA BAO TATU ZA WAZI SIMBA

MATAJIRI wa Simba wamefurahishwa na matokeo ya suluhu waliyopata dhidi ya Yanga na kusema bila kambi yao ya nchini Afrika Kusini wangeweza kufungwa si chini ya mabao 3-0 na Yanga. Kabla ya matokeo hayo ya juzi Jumamosi pale Uwanja wa Taifa, Simba ilikuwa Afrika Kusini ambako iliweka kambi ya siku nane kujiandaa na mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ambao ulimalizika suluhu. Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji ‘KD’, alisema kikosi chao kilikuwa katika hali mbaya ya kuweza kupoteza vibaya mechi dhidi ya Yanga na wasingefanya jitihada hizo wangejikuta wanapata kipigo cha aibu. Dewji ambaye ndiye aliyekuwa mmoja wa waratibu wa kambi hiyo, alisema Yanga kabla ya mchezo huo walikuwa katika morali nzuri kuliko Simba. Alisema kambi na gharama mbalimbali walizoziingia zimewagharimu zaidi ya Dola 350,000 ambazo ni sawa na Sh58 milioni. “Hatukuwa katika hali nzuri, tulilazimika kutumia akili hiyo ya haraka kuinusuru klabu kupata kipigo cha aibu maana tuliangalia timu yetu kulinganisha na Yanga na kubaini endapo tusingeandaa ile kambi tungeweza kupata kipigo cha aibu cha si chini ya bao 3-0,”alisema Dewji. Matokeo hayo yamewakera mabosi wa Yanga waliokuwa wanataka ushindi kuziba kelele za Simba huku wachezaji kilio chao ni kukosa Sh80 milioni walizoahidiwa endapo wangeshinda huku Simba nao wakikosa Sh100 milioni ambazo wangepewa kama wangeishinda Yanga. “Tulipambana sana hasa sisi mabeki, lakini tatizo lilikuwa mbele katika umaliziaji tu, tulikuwa tunalala na fedha uongozi ulituletea Sh80 milioni taslimu na ukatuhoji nani akabidhiwe lakini ndiyo hivyo tumechemsha,” alisema kwa huzuni beki mmoja wa Yanga.

CRD:Mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment