Saturday, October 25, 2014

HII NDIO HISTORIA YA MZIKI YA MAREHEME YP KUTOKA TMK WANAUME FAMILY

Wiki hii hapa tasnia ya bongofleva ilimpoteza msanii maarufu YP pichani ambaye anaunda kundi la TMK Wanaume Family.Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Yessaya Ambikile alifariki usiku wakuamkia Jumanne katika hospitali ya Temeke.
Said Fella ambaye ni meneja wa kundi hilo amesema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kifua kwa muda mrefu na ndo kitu ambacho kimechukua uhai wake.
Historia yake katika muziki:
Saidi Fella anasema kuwa alikutana na marehemu YP kwa mara ya kwanza mwaka 2004 katika ukumbi wa King Palace huko Temeke.Baadae kulikuwa na shoo ya TMK Wanaume Family katika ukumbi wa Luxury Pub marehemu akamfata akaomba amsaidie kimziki, ndipo Fella akamwambia amwimbie, akamwimbia wimbo wake uliokuwa unaitwa ‘Saidali’ na huo ndo ukawa mwanzo wakuitwa kwenye kundi hilo. Alivyofika kwenye kundi baada ya kumwambia Juma Nature kuhusu kipaji cha marehemu, Nature akamwambia kama yeye Fella ameona marehemu ana uwezo basi ni sawa apewe nafasi katika kundi hilo.

Mwaka 2005 marehemu pamoja na msanii mwingine wa kundi hilo Y Dash akatoa wimbo wao wa kwanza ‘Shemsa’ ambao ulifanya vizuri na kumtambulisha msanii huyo kwenye tasnia ya muziki.Kutokana na sauti ya marehemu kuendana na msanii mwenzake Y Dash wakatoa wimbo mwingine uliokuwa unaenda kwa jina la ‘Pumzika’.

Said Fella aliendelea kueleza kuwa marehemu alitoa wimbo ulioenda kwa jina la ‘Mapengo matatu’ ambao ni wimbo alioimba kutokana na kufiwa na baba yake,mama yake na mdogo wake.Mwaka 2006 marehemu pamoja na Y Dash ambaye kwasasa yuko nchini Afrika Kusini wakatoa album ya pamoja waliyoipa jina la ‘Mapengo matatu’.
Baada ya hapo marehemu akaendelea kushiriki kwenye kazi zingine za wasanii wa kundi la Tmk Wanaume Family na kazi za kundi kama ‘Twende zetu’ , ‘Dar mpaka Moro’, ‘Kichwa kinauma’ na nyingine nyingi.

Mwaka 2008 marehemu aliamua kuondoka katika kundi hilo na msanii mwenzake Y Dash pamoja na Jebby wakaenda kundi lingine ambalo walilipa jina la TMK Unity.Said Fella anasema mwaka 2010 msanii huyo alimtafuta nakumuomba kurudi katika nafasi yake tena ndipo alipomkubalia nakuwa kwenye kundi hilo mpaka kifo chake.Baada yakurudi TMK Wanaume Family nyimbo ambazo alizoshiriki marehemu nakufanya vizuri ni ‘Kichwa kinauma’, ‘Tunafurahi’ ya Mh Temba na Chegge.

Meneja huyo wa kundi hilo anasema kuwa kundi hilo limepata pengo kwasababu toka mwanzo kabla wakati TMK Wanaume Family kuvunjika msanii huyo alikuwa ni kati ya wale wasanii 11 wa mwanzo.Said Fella alifanunua kuwa alikuwa akianza Juma Nature,Chegge,Kr,Mh Temba na wengine na yeye YP anakuwa na namba.Kitu kingine alisema kuwa watamkumbuka YP kwa ucheshi na ubunifu wa staili za kucheza. “Yaani zile staili zote za TMK Wanaume Family kama mapangashaa nyingi alikuwa akizibuni marehemu pamoja na Kr, alikuwa ni mtu anayependa kucheza, mtu wakutengeza step”, Said Fella.Alieleza kuwa kazi ya mwisho ya kundi marehemu kurekodi ilikuwa ni mwezi uliopita katika studio za Sound Crafters.

Marehemu,Mh Temba na Chegge
Pia msanii wa kundi hilo Chegge alimzungumzia marehemu nakusema kuwa alipatwa na uchungu hadi anajikuta analia kwasababu watu wengi walikuwa wakizifananisha sauti zao na ndo maana alipenda kumshirikisha kwenye nyimbo zake.Msanii mwingine wa kundi hilo Mh Temba alisema kuwa atakumbuka ucheshi wa marehemu na pia ubunifu wake katika kutunga viiitikio(chorus) za nyimbo. “Kwakweli TMK Waunaume Family tumepoteza jembe.

Marehemu Yessaya Ambikile alizikwa jUZI katika makaburi ya Chang’ombe Maduka mawili alizaliwa tarehe 10 November mwaka 1986 jijini Dar es salaam akiwa ni mtoto wa kwanza, kisha akapata elimu ya msingi katika shule ya msingi Keko Magurumbasi.Baada yakumaliza elimu ya msingi marehemu hakuendelea na masomo akaanza kujishughulisha na muziki mpaka kifo chake.Marehemu ameacha mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka 8 pamoja na mzazi mwenzake ambaye alikuwa ana mpango wakufunga ndoa hivikaribuni.
Mungu ampuzimshe kwa amani YP.

0 comments:

Post a Comment