Monday, September 01, 2014
|
STRAIKA aliyesaini mkataba wa miezi sita na
Simba, Emmanuel Okwi, amepewa masharti
magumu ambayo asipoyatekeleza
yatamgharimu.
Viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba
wameamua kumshupalia mchezaji huyo
kutokana na rekodi zake za usumbufu wa mara
kwa mara ikiwamo kwenda kwao na kuchelewa
kurudi kambini.
Akizungumza na Mwanaspoti Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Zacharia Hans Poppe, amesema
wanaelewa tabia za Okwi na wamekaa naye na
kumpa masharti kwamba anatakiwa kubadilika
kwa vile nafasi waliyompa ndiyo ya mwisho
vinginevyo hawataweza kumvumilia.
Bosi huyo aliyemtambulisha Okwi mwishoni
mwa wiki iliyopita, alisema wamemsisitiza Okwi
kujituma na kuimarisha kiwango chake kwa
muda huu ili arudi kwenye fomu aliyokuwa
nayo siku za nyuma kwani Simba ni timu
kubwa na haitetemekei umaarufu wa mchezaji.
Alisema Simba waliyoisajili sasa inaweza
kufanya makubwa bila kumtegemea Okwi na
ndiyo maana wamempa mkataba ambao
utamruhusu kuondoka kama akipata timu
popote.
“Tunatambua hilo la tabia yake, kila kitu kipo
wazi tumemweleza kwamba tunamkaribisha
katika timu yetu, lakini anatakiwa kuangalia
maisha yake yalivyokuwa kila timu aliyokwenda
na sasa hii nafasi tuliyompa ni kama nafasi ya
mwisho kwake kutakiwa kujirekebisha,” alisema
Hans Poppe.
“Hatukuwa tunamuhitaji sana Okwi katika timu
yetu lakini kwa kuwa alikuja kutuomba
tukalazimika kumkubalia, sasa tumemweleza
kwamba hatuna mchezaji anayejiona ni
muhimu zaidi kuliko wengine. Simba ya sasa
kila mchezaji ni muhimu.
“Hata yeye mwenyewe ameliona hilo juzi katika
mechi yetu na amekiri kwamba akizembea
anaweza kuishia benchi kutokana na uwezo wa
wachezaji wetu wa sasa.
“Amejionea mwenyewe kwamba tunaweza
kufanya makubwa bila yeye, sasa hilo lipo
mikononi mwake.”
Simba juzi Jumamosi usiku iliwachapa KMKM ya
Zanzibar mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki.
Mafowadi wa Simba wamewapiku wa Yanga
kwenye ufungaji wa magoli kwenye michezo ya
kirafiki visiwani Zanzibar baada ya timu zote
kucheza michezo mitatu mitatu huku Simba
ikishinda kwa mzabao wakati Yanga ikiambulia
matano.
Kwa upande wa Simba, mchezo wa kwanza
ulikuwa ni dhidi ya Kilimani City ambapo Simba
ilishinda mabao 2-1, wafungaji walikuwa
Shabani Kisiga pamoja na Haroun Chanongo. |
0 comments:
Post a Comment