Tuesday, August 05, 2014

Trafiki FEKI Aibua Mazito.....Akutwa na Leseni 40, Radio Call na Pea 7 za Jeshi la Polisi

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, jana imelitolea ufafanuzi sakata la kukamatwa kwa askari 'feki' wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki), katika kata ya Chamazi, Mbagala Majimatitu, Wilaya ya Temeke, jijini humo.

Mtuhumiwa huyo, Bw. Robson Emmanuel (30), alikamatwa Agosti 2 mwaka huu, akijifanya Ofisa wa Polisi katika kikosi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema mtuhumiwa aliwahi kuwa mwajiriwa wa jeshi hilo kuanzia mwaka 2000 akiwa na namba F2460 lakini alifukuzwa kazi kwa fedheha Machi 3 mwaka 2014, Kibaha, mkoani Pwani akiwa na cheo cha Stesheni Sajenti.

"Katika uchunguzi wetu, tumebaini mtuhumiwa alikuwa akijitambulisha kama askari, hivyo alifanikiwa kuwatapeli wananchi wengi na kujipatia kiasi kikubwa cha fedha kwa njia za udanganyifu," alisema.

Aliongeza kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa amevaa sare za jeshi hilo na cheo cha Stesheni Sajenti pia alikutwa na gari aina ya Cresta namba T 723 BAK yenye rangi nyeupe ambayo alilitumia kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kutapeli.

"Katika gari hilo, polisi walipekua na kukuta radio call moja yenye namba GP380 aina ya Motorola, leseni za udereva 40, stakabadhi mbili za Serikali zenye namba A0531562 na A1672464, police loss report mbalimbali, kofia, beji, ratiba ya mabasi yaendayo mikoani na vitu vingine mali ya Jeshi la Polisi.

"Pia mtuhumiwa alipekuliwa nyumbani kwake ambapo polisi walikuta sare za jeshi hilo rangi ya kaki pea nne, pea tatu ambazo ni sare za Kikosi cha Usalama Barabarani, koti moja la mvua la kikosi hicho, reflector 8 za kuongozea magari, kofia, mikanda ya jeshi na vyeo vitatu vya Stesheni Sajenti," alisema Kamishna Kova.

Katika hatua nyingine, Kamishna Kova alisema jeshi hilo linawashikilia majambazi wawili kwa tuhuma za kujihusisha na unyang'anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Julai 30 mwaka huu, eneo la Makumbusho Kijitonyama kutokana na msako mkali wa jeshi hilo.

"Watuhumiwa hawa baada ya kupekuliwa majumbani mwao, walikamatwa na bastola mbili, moja aina ya Grock 17 yenye namba B019259 iliyotengenezwa nchini Czech ikiwa na risasi 13 ndani ya magazine, nyingine aina ya Chinese iliyofutwa namba zake ikiwa na risasi moja ndani ya magazine," alisema.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Fredy Steven (25), ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Kiwalani na Irene Nyange (36), mfanyabiashara na mkazi wa Kijitonyama ambapo uchunguzi unakamilishwa ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani wakati wowote.

Kama bado ujaungana nasi ili kila tukipata habari zikufikie punde tuziwekapo mtandaoni  BONYEZA HAPA 

0 comments:

Post a Comment