Thursday, August 07, 2014

Shemeji wa Rais Mstaafu Zanzibar ( Mansour Yussuf Himid) Apandishwa Kizimbani na kusomewa mashitaka matatu

Shemeji wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Aman Abedi Karume, Mansour Yussuf Himid, anaendelea kusota rumande baada ya jana kusomewa mashtaka katika Mahakama ya Mkoa wa Vuga kumiliki silaha kinyume na sheria.

Masour alifikishwa mbele ya Hakimu Khamis Ramadhan Abdallah wa mahakama hiyo jana chini ya ulinzi mkali wa polisi na usalama wa taifa na kusomewa mashtaka matatu ambayo yote aliyakana.

Kosa la kwanza kwa mujibu wa muendesha mashataka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Raya Mselem, ni kumiliki silaha aina ya bastola yenye namba F 76172W kinyume na kifungu namba 6 (3) na 34 (1)(2) cha sheria ya silaha na risasi ya mwaka 1991 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 223.

Mwendesha Mashtaka  huyo  akisaidiwa na Maulid Ali alitaja makosa mengine yanayomkabili Mansoor kuwa ni, kupatikana na risasi 295 kinyume na kifungu  cha 6 (3) na 34 (1) (2) sheria namba 7 ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kosa la tatu ni kupatikana na risasi za bunduki aina ya Shotgun 112 kinyume na kifungu cha 34 (1) (2)  sheria ya risasi na silaha  namba 2 ya mwaka 1991.

Baada ya kusomewa mashitaka, Hakimu wa makama hiyo aliamuru mshitakiwa huyo arejeshwe rumande hadi Agosti 18 mwaka huu kutokana na kosa la kwanza kutokuwa na dhamana na makosa mengine kuhitaji kuombewa dhamana.

Kwa upande wake wakili wa mshitakiwa huyo Omar Said Shaaban aliyekuwa na msaidizi wake Gaspa Nyika, alisema anakusudia kupeleka ombi la dhamana Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Mansor ambaye aliwahi kushika nyazifa mbalimbali katika serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na CCM kabla ya kuvuliwa uanachama, alikamwa Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Chukwani nje kidogo ya mjini wa Zanzibar.

 HABARI ZINGINE ZIPO HAPA 

0 comments:

Post a Comment