LIVERPOOL, ENGLAND
LIVERPOOL! Achana na moto wao. Wamepania kweli kweli mwaka huu. Imetumia pesa nyingi na sasa inataka matumizi hayo yavuke Pauni 100 milioni.
Baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini ikifanikiwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa imekuwa bize kwenye kukisuka kikosi chake na kumwaga pesa kama njugu kuhakikisha hilo linatimia.
Baada ya kuwanasa wachezaji sita hadi sasa, miamba hao wa Anfield wamemtuma Mkurugenzi wao, Ian Ayre, kwenda kumaliza dili za kuwanasa wakali wawili; Alberto Moreno na Javi Manquillo, kitendo kitakachowafanya kutimiza Pauni 100 milioni katika matumizi ya usajili kwa mwaka huu pekee.
Imeelezwa kwamba Liverpool imekubali kutoa Pauni 20 milioni kumsajili Moreno anayechezea Sevilla na ikijadili mkopo wa kumchukua beki wa kulia wa Atletico Madrid, Manquillo, lakini mkataba wake ukiwa na kipengele cha kulipa Pauni 6 milioni kama watavutiwa naye na kutaka kumbeba kwa jumla.
Hadi sasa Liverpool imetumia pesa nyingi kwenye usajili. Imemnasa Rickie Lambert kwa Pauni 4 milioni kutoka Southampton kabla ya kuivamia tena klabu hiyo na kumnasa Adam Lallana kwa Pauni 25 milioni.
Kisha ilitumia Pauni 10 milioni kumnasa staa wa Bayer Leverkusen, Emre Can kabla ya kwenda na Pauni 20 milioni za kumnasa Lazar Markovic kutoka Benfica.
Wakati mashabiki wa timu hiyo wakidhani kwamba Liverpool itakuwa imefunga kazi, kocha Brendan Rodgers alifungua tena pochi lake na kutoa Pauni 20 milioni kumnasa Dejan Lovren kutoka Southampton.
Fowadi mwenye asili ya Kenya, Divock Origi, ametua Liverpool kwa Pauni 10 milioni kutoka Lille, lakini mchezaji huyo aliyeamua kuchukua uraia wa Ubelgiji atabaki kwa mkopo kwenye klabu yake hiyo ya Ufaransa hadi mwakani.
Hadi sasa, Liverpool imetumia karibu Pauni 90 milioni kwa nyota hao Lallana, Lambert, Lovren, Emre Can, Markovic na Origi huku ikiwa imeuza mchezaji mmoja tu, Luis Suarez, kwa Pauni 75 milioni.
Kama bado ujajiunga nasi ili kila nikipata habari zikufikie kirahisi punde niziwekapo mtandaoni BONYEZA HAPA
0 comments:
Post a Comment