Sunday, August 31, 2014

Beki hii ya Simba, mh!

KOCHA wa Mafunzo ya Zanzibar, Hemed Morocco, amesema kuwa kikosi cha Simba kinaendelea kuimarika hasa safu ya viungo na washambuliaji huku akidai bado kuna tatizo kubwa katika safu ya mabeki hasa beki ya pembeni. Juzi Jumatano Mafunzo ilicheza na Simba katika Uwanja wa Amaan ambapo iliambulia kipigo cha mabao 2-0 ila kocha huyo alidai kuwa alikuwa anakiangalia tu kikosi chake kwani bado hajaanza kazi rasmi. Morocco alisema kuwa Simba wana timu nzuri ila kocha Patrick Phiri anatakiwa kufanya marekebisho haraka hasa nafasi hiyo ili isije ikamgharimu katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu ujao. “Ukiiangalia Simba ya sasa ni tofauti na ya msimu uliopita, nafasi ya kati na mbele wanacheza sana kwa kuelewana na wapo vizuri kuliko nafasi ya nyuma, sasa hilo ni tatizo ambalo kocha anatakiwa kulirekebisha,” alisema. “Kwa upande wa timu yangu ni vigumu kuzungumzia mapungufu yake kwani katika mechi hiyo nilikuwa naangalia tu kazi ya kuifundisha timu hiyo inaanza rasmi wiki ijayo, lakini kikubwa nampongeza Phiri kwa kuitengeneza upya Simba.” Katika mechi hiyo ya kirafiki, safu ya ushambuliaji ya Simba iliongozwa na Amissi Tambwe pamoja na Shaban Kisiga ambaye pia anacheza nafasi ya kiungo. Viungo ni Amri Kiemba, Pierre Kwizera, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Haruni Chanongo huku mabeki akiwatumia Issah Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Joram Mgeveke, William Lucian ‘Gallas’ huku golini akisimama Ivo Mapunda.credit mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment