Friday, August 08, 2014

ABDI BANDA AWAINGIZA SIMBA SC ‘CHOO CHA KIKE’

Katibu Mkuu wa Coastal Union,Kassim El Siagi akiwaonesha wanahabari baadhi ya vifungu vya mkataba wa Banda wakati wa mkutano na wanahabari jana klabuni Coastal Union .

Na Mwandishi Wetu, Tanga UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umekiri kupokea barua kutoka kitengo cha Wanasheria (Maleta & Ndumbaro Advocate cha Dar) ikisema kuwa timu hiyo imeshindwa kumlipa Abdi Banda mshahara wa miezi mitatu mfululizo na kusema imevunja mkataba.

Akizungumza jana,Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi amekanusha na kuwa habari zilizoenezwa kwamba walishindwa kumlipa mshahara mchezaji huyo sio za kweli bali kilichotokea ni kwamba Banda alifundishwa na watu wajinga asichukue mishahara yake ya miezi mitatu ili kukipa hadhi kipengele hicho cha sheria kilichopo kwenye mkataba wake, “Akinukuu kipengele cha ibara ya 3(3.2)(1) cha mkataba wa Banda kinachosema kuwa ikiwa klabu imeshindwa kumlipa mchezaji mishahara yake ya miezi mitatu mfululizo basi mkataba wa mchezaji huyo na klabu umevunjika “Alisema El Siagi.

Alisema alichokifanya mchezaji Banda ni kukwepa kuchukua mishahara yake makusudi ili ionekane kwamba hakulipwa miezi mitatu . El Siagi alisema alichokifanya ni mambo mawili, jambo la kwanza ni kudanganya wanamichezo hapa nchini na klabu yake ya Coastal Union ili aipatie fedha Klabu ya Simba ambapo huo ni Wizi wa kutumia hila.

Alisema la pili ni kitendo cha kusaini mkataba Simba wakati akijua ana mkataba na Coastal Union ambao unatarajiwa kuishia Juni 2016. Katibu huyo alisema ni makosa makubwa mchezaji huyo kusaini mikataba miwili tofauti katika kipindi cha msimu mmoja kwa sababu atakuwa amevunja taratibu za mikataba kutokana na kuwa mchezaji hawezi kuwa na mikataba miwili kwa wakati mmoja.

Aidha alisema kutokana na mchezaji huyo kudanganya na kukiuka utaratibu wa mkataba, Uongozi wa Coastal Union umejipanga kumchukulia hatua kali mchezaji huyo ikiwemo hatua za kinidhamu.

Katibu huyo alisema anashangazwa kuona kuwa klabu ya Simba yenye viongozi wazoefu kwenye masuala ya mpira wanafanya makosa kama hayo kwa kutokufuata taratibu za kiusajili.

“Kanuni za shirikisho la soka Dunia (FIFA) na Shirikisho la soka nchini (TFF) zinasema mchezaji hawezi kuzungumza na timu yoyote wakati akiwa ndani ya mkataba mpaka labda awe amebakiza miezi sita kwenye mkataba wake ndio anaruhusiwa kuzungumza na uongozi wa klabu nyingine.

Aliongeza kuwa iwapo mchezaji akiwa amebakiza mwaka mmoja basi klabu na klabu ndio zinaruhusiwa kuongea na sio mchezaji hivyo Banda bado ana miaka miwili Coastal Union ambayo imebaki hivyo Simba walichotakiwa kufanya ni kuzungumza na uongozi wa Coastal union ili kumnunua mkataba wake badala ya kurubuniwa na kauli hafifu za kiudanyanyifu.

Katibu huyo alisema kwa kufanya hivyo Coastal Union kupitia wanasheria wake ,Divine Chambers Advocates & Hamidu Mbwezeleni wanajipanga kuwaandikia barua shirikisho la soka nchini (TFF) pamoja na Simba ili kudai fidia ya ukiukaji wa taratibu hizo.

Alieleza kuwa tayari Coastal Union wamemtumia mwanasheria wa Banda majibu ya barua yake kupitia mwanasheria Divine Chambers Advocates ya Mjini Tanga.

Kama bado ujaungana nasi BONYEZA HAPA 

0 comments:

Post a Comment