Friday, July 11, 2014

TAASISI YA SAKA TIBA MPASUKO YA KATIBA

Taasisi inayojishughulisha na Utafiti wa Sera za Umma Zanzibar (ZIRPP) imeunda kamati ya watu sita ya kuwaunganisha wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar ili kuondoa tofauti zao za kiitikadi zilizosababisha mgawawiko mkubwa.

Taasisi hiyo chini ya mwenyekiti Mohamed Yussuf imefikia azimio hilo katika mdahalo wa wazi wa Rasimu ya Katiba uliofanyika jana mjini Unguja na kuhudhuriwa na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wajumbe walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni aliyekuwa mwakilishi wa Chambani (CUF), Abbas Juma Muhunzi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar, Enzi Talib Aboud aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Ali Hassan Khamis, Mselem Khamis na Ali Abdallah Suleiman.

Kamati hiyo itawashirikisha wazee 10 kutoka Pemba na Unguja ambao watakutana na viongozi wa dini na watu mashuhuri, baadaye kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Moahamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.

Makundi mengine watakayokutana nayo ni baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 wa Bunge la Katiba, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Wabunge wa Bunge la Muungano na kamati ya uongozi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Itakumbukwa kuwa mjadala wa Muungano uliwagawa wajumbe hasa kuhusu idadi ya Serikali na wajumbe kutoka Zanzibar walijikuta katika mtanziko, huku wale wa CUF wakipigania Zanzibar yenye mamlaka kamili na wale wa CCM wakipigania serikali mbili. Kutokana na hali hiyo, wajumbe kutoka CUF waliungana na Chadema na NCCR- Mageuzi na wachache kutoka kundi la 201 kutaka rasimu iliyowasilishwa ndiyo ijadiliwe, huku wale wa CCM na baadhi kutoka kundi la 201 wakisimamia muundo wa Serikali mbili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo aliyehudhuria mdahalo huo, alisisitiza umuhimu wa kubadili mfumo wa Muungano na haja ya Zanzibar na Tanganyika kila moja kupata mamlaka kamili. “Tatizo ni Serikali ya Tanganyika kuendelea kujificha kwenye koti la Muungano.

Tunataka ionekane mahali ilipo, kila upande uwe na serikali yake, baadaye kuwe na Serikali ya Muungano itakayoshughulikia mambo ya Muungano, hilo ndilo suluhisho na tiba,” alisema Moyo.

Kwa upande wake Ali Hassan Khamis alisema mpango wowote wa kudai mamlaka kamili ya dola ndani ya dola moja iliyopo sasa ni sawa na kuvunja Muungano na kwamba yeye binafsi asingependelea jambo hilo litokee kwani linaweza kuligharimu Taifa.

Kama unataka upate habaru.kilahisi zaid punde zinapo tufikia like page yetu  BONYEZA HAPA 


UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon

0 comments:

Post a Comment