Monday, July 28, 2014

Matajiri wa Simba wafanya usajili wa kihistoria

JANA Jumapili jioni, Simba ilitarajia kumpokea straika, Paul Kiongera, kutoka KCB ya Kenya, lakini awali mchana matajiri wa klabu hiyo wakamilisha usajili wa kihistoria kwa kumnasa Shaaban Kisiga ‘Marlone’.

Usajili huo unaingia katika rekodi kwani umemnasa mchezaji wa hadhi kubwa lakini kwa dau la Sh5 milioni tu.

Katika hali ya kawaida, mchezaji mwenye hadhi ya Kisiga husajiliwa kwa kati ya Sh10 milioni hadi 30 milioni. Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba, Kisiga alisema hajarejea klabuni hapo kama jina tu bali kwa ajili ya kuifanyia mambo klabu hiyo ya Msimbazi lakini kikubwa anaomba ushirikiano.

“Ni kweli nimeshamalizana na Simba, kikubwa ninachoweza kusema, halijarudi jina Simba bali nimerudi nikiwa nimejipanga kwa ajili ya kufanya kazi kuona klabu inafanya vizuri kwenye ligi na michuano mingine tutakayoshiriki,” alisema Kisiga ambaye msimu uliopita aliichezea Mtibwa kwa mafanikio.

“Nina hamu, nina majukumu mazito kuhakikisha nafanya kazi niliyokusudia, hivyo mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi. Kikubwa ni ushirikiano kwa wachezaji wenzangu na viongozi.” Kisiga amesajiliwa baada ya kumaliza mkataba na Mtibwa na mtu aliye karibu naye amedokeza kuwa ameweka kibindoni fedha za usajili Sh5 milioni na atakuwa akipokea mshahara wa Sh1.5 milioni.

Wakati huohuo, jana Jumapili jioni, Mkenya Kiongera aliyetoka KCB ya Kenya, alitarajiwa kusaini mkataba na Wekundu wa Msimbazi hao na mambo yakienda vizuri, Elius Maguli na Mrundi Kwizera nao watasaini.

Source mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment