Meneja wa klabu bingwa nchini Uingereza Man city, Mannuel Luis Pellegrini ametangaza mikakati aliyojiwekea kwa msimu ujao wa ligi ambao utaanza kutimua vumbi lake August 16.
Pellegrini, amesema baada ya kutwaa ubingwa wa nchini Uingereza msimu uliopita, amedhamiria kusonga mbele zaidi kwa kusaka mafanikio tofauti na hayo aliyoyapata katika msimu wake wa kwanza huko Etihad Stadium.
Akiwa nchini Marekani ambapo kikosi chake kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi, meneja huyo kutoka nchini Chile amesema dhamira yake kubwa kwa sasa ni kuhakikisha anaipa heshima Man city kwa kutwaa ubingwa wa barani Ulaya ambao unashikiliwa na Real Madrid.
Pellegrini, amesema anaamini anaweza kufikia malengo aliyojiwekea baada ya kikosi chake kuonyesha uwezo mzuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita, ambapo kilifanikiwa kucheza hatua ya 16 bora kabla ya kutolewa na FC Barcelona kwa jumla ya mabao manne kwa moja.
Katika hatua nyingine Mannuel Luis Pellegrini amesema bado hajamaliza kufanya usajili wa wachezaji ambao watakiongezea nguvu kikosi chake, kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao.
Amesema kwa sasa anaitumia michezo ya kirafiki kuangalia mapungufu yaliopo kikosini kwake, na akibaini chochote ambacho huenda kitamkwamisha msimu ujao, atafanya mabadiliko kwa kumsajili mchezaji atakaeona anafaa
Kikosi cha Man City alafajiri ya leo kilicheza mchezo wa kujipima nguvu huko nchini Marekani dhidi ya Sporting Kansas City na kufanikiwa kupata ushindi wa mabao manne kwa moja.
Mabao ya Man city katika mchezo huo yamepachikwa wavuni na Bruno Zuculini, Dedryk Boyata, Aleksandar Kolarov pamoja na Kelechi Iheanacho huku bao la kufutia machozi upande wa wenyeji likifungwa na Charles Sapong.
0 comments:
Post a Comment