Saturday, July 26, 2014

Kundi lingine la uhalifu laibuka mkoani Dodoma....Vijana hao wanajiita "Wadudu wa Dampo

Kundi kubwa la vijana wanaojiita wadudu wa dampo limeibuka mjini Dodoma na kufanya matukio ya uhalifu huku likihusishwa na mauaji ya watu wanne yaliyotokea hivi karibuni.

Uwepo wa kundi hilo umezua hofu na taharuki kwa wakazi wa mji huo hasa nyakati za usiku kutokana na wingi wao huku wakitembea na silaha mbalimbali za jadi wakati wakitekeleza matukio ya uhalifu.

Kundi hilo lenye makazi yake kata ya Chang'ombe manispaa ya Dodoma linaratibu na kutekeleza matukio ya uhalifu kwa kuwavamia watu, kuwapiga na kuwapora pamoja na kuwabaka wanawake huku wakitumia silaha za jadi ikiwa ni mapanga, visu na mikasi.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Dodoma Lefy Gembe ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani amesema tayari kamati yake imeshajipanga kukisambaratisha kikundi hicho ili kisiendelee kuvuruga amani.

Diwani wa kata hiyo Rajabu Fundikira amekiri kuwepo kwa matukio hayo na kusema kuwa tayari ameshawasiliana na uongozi wa jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma na kutoa kikosi maalum kwa ajili ya kuimarisha ulinzi ambacho huzunguka usiku. Mwandishi amefanya mahojioano na mwenyekiti wa moja ya mitaa ambayo ni chimbuko la kundi hilo mkoani Dodoma, Mtaa wa Mazengo Changombe, Abdallah Mtosa ambaye amekiri kuwa kundi hilo lipo na limekuwa likifanya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya kata ya Chang'ombe.

Amesema kuwa Wadudu wa Dampo wamekuwa na vituo vyao ambapo hufanya uhalifu huo ambao ni katikati ya Chang'ombe na Nkuhungu sehemu ya wazi ambayo ina Makabuli ambapo hujificha na kuwateka watu wanaopita katika maeneo hayo.

0 comments:

Post a Comment