Kuwasili kwa wabrazil wawili katika klabu ya Yanga kumeweka rehani ajira za wachezaji Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kwasababu mmoja wao inabidi atemwe ili timu hiyo iweze kutimiza masharti ya kuwa na wacheza kigeni watano tu.
Lakini kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kwamba Kiiza ndio atatemwa na kumpisha mshambuliaji Genilson Santos ‘Jaja’ ndani ya listi ya wachezaji wa kigeni. Mwanaspoti linaripoti – YANGA ipo katika mchakato wa kuachana na Hamis Kiiza (pichani) ili nafasi yake achukue Genilson Santos ‘Jaja’, lakini hawajamwambia chochote na hata wakizungumza nae wanazuga tu kama hamna kitakachotokea.
Pia straika huyo wa Uganda ameshashtukia dili na amesema kwamba hana wasiwasi wowote kuhusu hilo na anangoja kauli ya viongozi wake, ingawa Mwanaspoti linajua kwamba Simba wanamnyatia na SC Villa ya Uganda imeshafanya nae mazungumzo ya awali wanasubiri Yanga impe chake wamnase.
Hadi sasa Yanga ina mkataba na wachezaji sita raia wa kigeni lakini kanuni za Ligi Kuu ya Bara inaelekeza matumizi ya wachezaji watano tu wa kigeni, hivyo inalazimika kuachana na mmoja wa wanasoka hao.
Wachezaji wa kigeni wa Yanga ni Kiiza na Emmanuel Okwi (wote Uganda), Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite (wote Rwanda), Jaja na Andrey Coutinho wote kutoka Brazil. Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mmoja kati ya Okwi na Kiiza anatakiwa kuachwa lakini kura inaonekana kumuangukia Kiiza ambaye sasa yupo katika kikosi cha Uganda ‘The Cranes’ akijiandaa na mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika dhidi ya Mauritania.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Uganda, Kiiza alisema; “Kama Yanga wamepanga kuniacha waniambie tu haina shida, halafu nitajua jambo la kufanya. Sihofii lolote kuhusu uamuzi utakaochukuliwa na viongozi kwa maana soka ni ajira yangu.
”Kiiza alisema mkataba wake unaisha Mei mwakani hivyo kama Yanga ikitaka kuachana naye itabidi ivunje naye mkataba.
“Naamini bado nina uwezo mkubwa na nimeweza kuifanyia mambo mengi Yanga hivyo sina wasiwasi kama wataniacha nitakuwa sehemu nyingine lakini kwa sasa naheshimu mkataba wangu na Yanga kwani ni timu mwajiri wangu
0 comments:
Post a Comment