Saturday, July 12, 2014

January makamba amjibu Mokiwa na Jk

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema hawezi kubishana na Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa, kwa sababu ni kama baba yake.

January aliyasema hayo jana wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam. January ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga (CCM), alisema iwapo Askofu Mokiwa kwa mtazamo wake anaona staili ya unyoaji nywele ni sifa ya urais basi anawaachia waumini wake na Watanzania kupima wenyewe kauli hiyo.

Mbali na Mokiwa pia January alitumia nafasi hiyo kujibu kauli ya Rais Kikwete ambaye alimpa ushauri wa kusikiliza ushauri wa wazee kabla ya kufanya uamuzi wake. “Wako wazee wengi ndani ya CCM wa kuwaona na wengine nimekwishawaona na Rais Kikwete kwa nafasi yake ni refarii wa mchezo,” alisema January.

Alisema kutangaza kwake kugombea si kwamba anataka cheo cha urais kwani kwake urais ni utumishi. January alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Askofu Mokiwa kuzungumzia sifa za mgombea urais akisema nchi haiko tayari kuongozwa na wanyoa ‘unga’ (kipara) na kwamba wakati wa Tanzania kuongozwa na vijana haujafika.

Ingawa Mokiwa hakutaja moja kwa moja jina la January, lakini ndiye kijana pekee ambaye ametangaza nia ya kuwania urais na kudai ni wakati wa vijana kushika hatamu za uongozi. Wasomi nao wamshauri Baadhi ya wasomi nchini wamemtaka January kufuata ushauri aliopewa na Rais Jakaya Kikwete, asilazimishe kuwania nafasi ya urais kwa sababu wakati ukifika atapata.

Akiichambua kauli hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema haiwezekani kwa mtu kupewa nafasi ya uongozi kama hana uzoefu wa kazi. Dk. Bana alisema kutokana na hali hiyo ndio maana hata, Rais Kikwete alitengenezewa njia kabla ya kupewa jukumu la kuiongoza nchi.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Hajji Semboja alisema kauli ya Kikwete ni ya kiongozi mwenye hekima na busara. Alisema kila chama kina utaratibu wake wa kuchagua wagombea, hivyo alipaswa kufuata utaratibu huo kabla ya kutangaza hadharani.

Kauli ya Kikwete imekuja siku chache baada ya January kutangaza kuwania nafasi hiyo wakati akihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), wiki iliyopita.

Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Grace Shitundu na Veronica Romwald (Dar)

Kama bado uja like ukurasa huu ili kila tupatapo habari zikufukie kirahisi zaidi BONYEZA HAPA 


UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon

0 comments:

Post a Comment