Saturday, July 26, 2014

Giggs adai Van Gaal ni kama Ferguson

RYAN Giggs amepagawa. Amepagawa na kipigo cha mabao 7-0 ambacho Manchester United imetoa kwa LA Galaxy katika pambano la kirafiki Alhamisi asubuhi na amedai kwamba kocha Louis van Gaal anafanana sana kitabia na Sir Alex Ferguson.

Giggs alichaguliwa kuwa kocha msaidizi wa van Gaal mara baada ya Mdachi huyo kutangazwa kuwa kocha wa United Mei mwaka huu na baada ya kucheza chini ya Sir Alex Ferguson kwa zaidi ya misimu 20 amedai kwamba wawili hao wamefanana.

“Nadhani wamefanana na Fergie. Wana tabia moja inayowafananisha. Hilo linatoka katika mafanikio ambayo wamekuwa nayo. Wanataka wachezaji wajibu mapigo na wanataka heshima.” Alisema Giggs.

“CV yake inajionyesha yenyewe. Amefundisha timu kubwa na anatoka katika kazi ya mafanikio kombe la dunia hivi karibuni. Ameonyesha anachoweza kufanya. wachezaji wamejibu mapigo katika hilo. Katika kipindi kifupi nilichofanya kazi na Louis utaona ni kwanini ana mafanikio.” Aliongeza Giggs.

“NI mtu anayefundisha. Anataka kila kitu kiende sawa kuanzia dakika ya kwanza mpaka mwisho. Kila anachofanya kipo wazi, na kila mtu anaelewa vizuri. Ana njia za kipekee za kufikisha ujumbe lakini ni vizuri ukimuelewa kwa mara ya kwanza.” “Ni vitu rahisi lakini kama ukifanya makosa atakwambia hapo hapo na ukifanya vizuri atakwambia hapo hapo.

Unajua unachokifanya vibaya na unajua unachokifanya vizuri. Hajali wewe ni nani.” Giggs amewataka wachezaji wa United kurudisha heshima yao baada ya kumaliza nafasi ya saba msimu uliopita na kusababisha timu hiyo ishindwe kushiriki michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao. “Kuna wasiwasi kwamba ni wachezaji wachache walioweza kufikia viwango vyao msimu uliopita.

Sio wachezaji wabaya. Wote ni wazuri. Mambo hayabadiliki ndani ya usiku mmoja lakini nafasi ya msimu uliopita ilionyesha kuwa hatukufanya vizuri kwa mchezaji mmoja mmoja au kitimu.” “Njia ya kurudisha hali hii imeshaanza. Hakuna muda wa kupoteza. Kombe la dunia lilimaanisha kwamba hakuna muda wa kupoteza. Lakini juhudi za kurudisha heshima zinaanza sasa. Inabidi tuipate fomu ya mechi yetu ya mwisho dhidi ya Swansea.” BONYEZA HAPA 

Source mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment