Friday, July 25, 2014

Barabara hizi zitafungwa kwa ajili ya Mashujaa

Baadhi ya barabara za Jiji laDar es Salaam zitakazofungwa kwa muda kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watu watakaohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ni Lumumba, Uhuru n a Bibi Titi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki aliyasema hayo jana alipotembelea mazoezi yanayofanywa na wanajeshi katika viwanja hivyo.

Alisema itawekwa runinga katika maeneo muhimu ya Mnazi Mmoja kuwezesha kila mshiriki kupata fursa ya kuona vizuri matukio yanayoendelea na kusisitiza; "Napenda pia kuhimiza suala la usafi katika majumba yote yanayozunguka viwanja hivi vya Mnazi Mmoja kuleta taswira nzuri,

" Alisema maadhimisho hayo yataanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana, Mgeni rasmi katika kumbukumbu hiyo muhimu katika historia ya nchi ya kuwaenzi mashujaa walijitoa katika jitihada za kuikomboa nchi na kuilinda na kudumisha amani anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.

Tarehe ya leo imeteuliwa kuwa siku ya mashujaa Tanzania. Ni tarehe waliyopokelewa wanajeshi wetu- mashujaa waliokuwa vitani nchini Uganda.

Wanajeshi wetu walikwenda kazini kumnyoosha nduli Iddi Amini. Rais huyo wa zamani wa Uganda aliyejigamba kuwa na nguvu za kuchukua sehemu ya Ardhi ya Tanzania na kuifanya kuwa sehemu ya nchi yake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999), kwa kutumia vigezo vya "vita halali" just war ya St. Augustine of Hippo 354-430 alitangaza vita kwa kuzingatia sababu inayokubalika, kujilinda dhidi ya adui, na kupigana vita kwa uangalifu na kupunguza maumivu kwa wasio na hatia.

Vijana wa jeshi la Tanzania na nchi yote kwa ujumla tulishinda. Tunapokumbuka mashujaa wetu, watu wengi hufikiria tu wanajeshi na wapiganaji wengine waliolipigania Taifa letu.

Hapa utakumbuka watawala kama Mkwawa, Kimweri, Mirambo, Mputa, na wengine wengi. Ni vyema sana kuwakumbuka ndugu waliokuwa tayari kulilinda Taifa letu. Muhimu katika kumbukumbu hii ni suala zima la uzalendo. Watu wote tunaowatambua kama mashujaa, kwa namna fulani walikuwa na uzalendo mioyoni mwao.

Hawa ni sawa na watu tunao watambu kama watakatifu, watakatifu huitwa wadhambi waliotubu. Nawafananisha mashujaa katika nchi na watu wenye "utakatifu" unapowapima kwa vigezo vya uzalendo.

Kumbe tunapowaheshimu mashujaa wetu ni lazima tujitazame na kujipima uzalendo wetu. Mzalendo tunamtarajia kuwa mtu mwenye kuipenda kwa moyo wake wote nchi yetu ya Tanzania.

Katika hili kila mmoja na hasa wenye ofisi za Umma ama zozote zenye kutoa huduma kwa umma wa wanadamu, wanaalikwa kujipima, wanajali kwa kiasi gani maslahi ya wananchi walio wengi dhidi ya maslahi binafsi. Kiongozi anapopata fursa ya uongozi anatakiwa kufanya hivyo kwa niaba ya wananchi walio wengi; na ili aongoze vyema kuna mkataba unaomwelekeza kama anavyosema mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau(1712-1778) kwenye kazi yake ya The Social Contract (1762), kiongozi anafanya yale anayoelekezwa na wananchi na si anayotaka yeye; viongozi wangapi hivi leo hapa nchini wanazingatia anachosema mwanafalsa huyu.

Wengi hawafuati makubaliano baina yao na wananchi, na kwa hivi wanalazimika kuacha mamlaka kwa wananchi wengine ili waongoze kama anavyosema mwafalsafa mwingereza John Locke (1632-1704). Locke anasema kiongozi mzuri anatakiwa awe na kumbukumbu ya makubaliano yake na wananchi moyoni mwake, vinginevyo aachie mamlaka. Hivyo basi tunaweza kuwaenzi vizuri zaidi mashujaa wetu kwa kujitazama katika kioo na kuona kiwango cha uzalendo wetu kwa Tanzania yetu.

Asanteni Mashujaa wetu na Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

0 comments:

Post a Comment