Friday, August 15, 2014

ANGALIA PICHA ZA LUIS SUAREZ AKIFANYA MAZOEZI KWA MARA YA KWANZA NA TIMU YA BARCA

Akijiimarisha na staili ya Barca
Sualez akiwa katika tabasamu alipokuwa anafanya mazoezi na wachezaji wenzake
Kazi imeanza: Luis Suarez akifanya mazoezi na wachezaji wenzake wa Barcelona leo ijumaa akiwemo nahodha wa klabu, Xavi.

JOSE MOURINHO AGOMA KUANIKA SIRI KAMA ANAHITAJI NYOTA WENGINE

KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho amegoma kusema kama bado anahitaji wachezaji wengine Stamford Bridge majira haya ya kiangazi.

The Blues wamewasajili Filipe Luis, Diego Costa, Cesc Fabregas na Didier Drogba kwa dau la jumla la paundi milioni 75 na Thibaut Courtois amerejea klabuni baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo katika klabu ya Atletico Madrid.

Mourinho licha ya kudai kuwa ana furaha na kikosi chake, amemuambia Petr Cech kuwa yupo huru kuondoka. Hata hivyo, kocha huyo amesema bado anaweza kufanya usajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi kwasababu muda bado upon a itategemeana na hali halisi.

Aliwaambia waandishi wa habari; “Soko bado lipo wazi na uzoefu unatuonesha kuwa wakati soko lipo wazi huwezi kusema kitakachotokea.

Kama unajua wachezaji wako walikuwa katika kiwango fulani mara ya mwisho mwezi uliopita, hatuwezi kujua timu nyingine zinahitaji kufanya kitu gani kwa wachezaji wetu”. “Lakini ukweli ni kwamba nina furaha na kikosi changu. Nina furaha na timu yangu na mfumo unaniunga mkono” Inafahamika kuwa Chelsea imetuma maombi ya kumsajili mshambuliaji wa QPR, Loic Remy baada ya Didier Drogba kupata majeruhi ya kifundo cha mguu.

Pia dili la kumsajili mlinda mlango kinda Ivan Brkic linaelekea kukamilika. Mourinho alieleza kuwa amevutiwa na wachezaji alionao katika kikosi chake na amekiri kuwa timu yake itakuwa katika mbio za ubingwa msimu wa 2014/2015. “Tumeleta baadhi ya wachezaji muhimu tuliowahitaji katika kikosi chetu. Wachezaji hawa wametufikisha sehemu nyingine”.

“Ndio, sisi ni washindani wa ubingwa. Kama unanitaka nisema kama tutashinda ubingwa, siwezi, kwasababu ninaheshimu ushindani huu”. Chelsea itaanza mbio za ubingwa dhidi ya Burnley katika dimba la Turf Moor siku ya jumatatu.

 KAMA BADO UJAJIUNGA NASI BONYEZa HAPA 

HIKI NI KIKOSI MAALUM KITAKACHO MENYAMA NA MAGWIJI WA ZAMANI WA REALMADRID AGOSTI 23 UWANJA WA TAIFA

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM MAKIPA maarufu waliowahi kuwika nchini, Mwameja Mohamed na Manyika Peter wamejumuishwa katika kikosi cha Tanzania All Stars kitakachomenyana na magwiji wa Real Madrid ya Hispania, Agosti 23, mwaka huu.

Chini ya makocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ na Wasaidizi Freddy Felix Minziro na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Daktari Mwanandi Mkwankemwa na viongozi Mtemi Ramadhani, Hassan Mnyenye, Omar Gumbo na Hamisi Kisiwa kikosi hicho kitaingia kambini Dar es Salaam kujiandaa kwa mchezo huo wa Agosti 23, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wengine walioItwa ni mabeki Nsajigwa Shadrack, Mecky Mexime, Boniface Pawasa, John Mwansasu, Abubakar Kombo, George Masatu, Habib Kondo, Viungo Suleiman Matola, Shaaban Ramadhani, Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’, Yussuf Macho, Abdul Mashine, Abdul Maneno, Mao Mkami, Steven Nyenge, Madaraka Suleiman, Akida Makunda na Mtwa Kihwelo.

Washambuliaji ni Monja Liseki, Iddi Moshi, Dua Said, Emmanuel Gabriel, Said Maulid, Thomas Kipese, Nasor Mwinyi ‘Bwanga’, Edibilly Lunyamila, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Clement Kahbuka, Madaraka Suleiman na Akida Makunda.

Wachezaji waliotamba kuanzia La Liga, wakacheza ligi nyingine za Ulaya, Kombe la Ulaya, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia waliowahi kuchezea Real Madrid watakuja nchini Agosti 22.

Katika ziara hiyo, pamoja na kucheza mchezo wa kirafiki na kikosi maalum cha wachezaji nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kupanda mlima Kilimanjaro.

Real Madrid inakuja nchini kwa mwaliko wa kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Farough Baghozah. Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja na Real nchini ni pamoja na Wanasoka Bora wa zamani wa Dunia, Mfaransa Zinadine Zidane, Mreno Luis Figo na Mbrazil, Ronaldo Lima.

Magwiji hao wa Real tayari wamekwishafanya matangazo ya ziara yao nchini wakisema wana hamu mno ya kukanyaga ardhi ya Tanzania.

Kampuni ya Vodacom Tanzania ni miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza kudhamini ziara pamoja na Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza Bahari Beach. Wito umetolewa kwa makampuni zaidi kujitokeza kudhamini ziara hiyo ya kihostoria nchini.

Na mdadisiblog/festosaimon

 ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG HII ILA BONYA HAPA KUHUNGANA NASI 

#BringBackOurWema: Ujumbe wa Diamond umeonesha ni Wema ndiye anayehitaji kubadilika!

Tuseme na ule ukweli… Kila mmoja katika maisha ya uhusiano amewahi kuongea maneno kwa hasira kwa mpenzi wake na baadaye kuja kugundua kuwa yalikuwa makali kiasi cha kumuumiza mwenzi wake. Hii inatokea sana, na after all sisi wote ni binadamu na sijawahi kusikia kuna binadamu aliyewahi kuishi kwenye ulimwengu huu akatajwa kuwa alikuwa mkamilifu.

Udhaifu ni miongoni mwa sifa zetu wanadamu. Udhaifu huo ndio ulimfanya Diamond aandike ujumbe ambao kwa wengi umeonekana kama ni msumari wa moto kwenye moyo laini wa mpenzi wake Wema Sepetu.

Kabla ya kuanza kujudge mimi ni nani hadi niwajudge wawili hawa, naomba nimnukuu Akon ambaye hivi karibuni aliwahi kutoa maoni yake kuhusiana na tetesi za kuvunjika kwa ndoa ya Jay Z na Beyonce. Akon alisema: Ukiwa mtu unayejulikana na una uhusiano, uhusiano wako nao unakuwa wa umma. Hivyo usipofunguka kwa umma, ni kawaida wao kuongea vitu wanavyohisi vinaendelea.”

Akon alimaanisha kuwa uhusiano wowote wa watu wanaojulikana hugeuka kuwa uhusiano unaongaliwa na kila mtu. Mkiwa mastaa hamuwezi kuwa na uhuru tena.

Hivyo kwa muda mrefu mashabiki wa Wema na Diamond wamekuwa wakihisi kuna jambo lisilo sawa katika uhusiano wao. Mashabiki wa Wema waliamua kuanzisha kampeni ya #BringBackOurWema baada ya kuhisi kuwa ni Diamond pekee anayenufaika na uhusiano huo, huku career na CV ya Wema ikiendelea kushuka.

Wengi wanaamini kuwa Diamond amekuwa akitumia nguvu ya Wema kujiimarisha zaidi yeye. Ni kawaida hata hivyo kuwa mastaa wawili wakubwa wanapoungana, huwaangunisha pia mashabiki wao kuwa kitu kimoja. Na kwakuwa wote wawili kwa fani zao wana fanbase kubwa, muunganiko wao umetengeneza super fanbase.

Siku chache zilizopita niliandika makala kuhusu kufanana kwa mienendo ya Kim Kardashian na Wema Sepetu na nikadai kuwa tofauti yao ni jinsi Wema anavyoushusha ustaa wake kwa kukatika jukwaani kama dancer wa Diamond, wakati anatakiwa ‘kubehave’ kama first lady wa mwanamuziki anayependwa zaidi Afrika Mashariki kwa sasa.

PICHA: DIAMOND NA WEMA NI KAMA KANYE WEST NA KIM KARDASHIAN LAKINI…

Hicho, na mengine ndicho kimekuwa chanzo cha kuanzishwa kwa kampeni ya #BringBackOurWema.

Kwakuwa lawama nyingi zimetupwa kwa Diamond kuwa ndiye chanzo cha kuporomoka kwa heshima ya Wema huku wengi wakidhani kuwa staa huyo wa muziki haonekani kutoa msaada wowote kwa mwandani wake, ilikuwa ni lazima Diamond ajibu kwanini hali iko hivyo.

Niliwahi pia kuandika makala ya kumshauri Diamond atumie connection zake kumtafutia mashavu ya kimataifa Wema Sepetu.

KWANINI WEMA SEPETU HATUMII UMAARUFU WA DIAMOND KUTAFUTA FURSA YA KUFANYA FILAMU ZA KIMATAIFA?

Hata hivyo inaonekana Diamond aliuzingatia ushauri huo kwakuwa mwezi June mwaka huu alidai kuanza kumuunganisha na waigizaji wa Ghana.

DIAMOND AMUUNGANISHA WEMA SEPETU KUFANYA FILAMU NA WAIGIZAJI WA GHANA

Kama alivyosema Akon kuhusiana na ukimya wa Jay Z na Beyonce kuhusiana na ndoa yao kiasi cha kuwafanya watu wawe na ‘speculations’ cha kile wachohisi kinaendelea, ndivyo hivyo ingekuwa kwa Diamond kama angeamua kutumia ukimya kama jibu la kampeni hiyo.

Bahati mbaya, majibu ya Diamond kupitia Instagram yamekuwa makali kiasi cha kuwashtua wengi na kuona kama kamkosea heshima mpenzi wake. Kwakuwa sitaki kuonekana kama namhukumu Diamond kwa kile alichoandika, ningependa kuongea kwa lugha ya busara kadri iwezekanavyo, na isitoshe nimegusia suala la ‘udhaifu’ na ‘ubinadamu’ katika aya zangu za mwanzo.

Diamond ametumia kauli nzito na ya hasira kidogo katika kuwajibu vinara wa kampeni hiyo. Si jambo la busara kumuita mtu umpendaye kwa kuandika ‘msanii wenu’ baada ya jina lake, pale alipoanza kwa kuandika: Nafikiri ningewaona kweli Mnaakili na Mapenzi ya dhati kwa ‘Msanii wenu’. Ingekuwa vyema kama angeandika; Nafikiri ningewaona kweli Mnaakili na Mapenzi ya dhati kwa ‘Wema Sepetu’. Again, hizo ni hasira tu na ndio maana aliamua kuifuta post hiyo.

Kwa maelezo aliyoyatoa staa huyo, imebainika wazi kuwa ni Wema ndiye aliyeamua kuishi hivyo na pengine ameridhika na hatua aliyofikia. Inavyoonekana Diamond hapendwezi na muenendo na maisha ya mpenzi wake hasa kwa kudai anaendekeza urafiki na watu wanaopenda anasa na kula bata.

“Mngemshauri apunguze mashoga wapenda anasa na apunguze starehe zisizo na faida, wenda ingemsaidia pesa kuzitumia kwenye kufanya kazi na kuleta maendeleo badala ya kuwapa viwanda vya pombe,” yanaendelea kusomeka majibu ya Diamond. Maelezo hayo yanaeleweka wazi kuwa Wema amekuwa ni mtu wa starehe na kula raha na marafiki zake (Aunty Ezekiel haikwepi hii sentensi, inamhusu). Kwa kauli ya Diamond, Wema anaonekana kuendekeza ulevi kwa kutumia fedha anayopewa na mchumba wake.

“Mimi kama bwana, wajibu wangu ni kuhakikisha mpenzi wangu anakula vizuri, anavaa vizuri, analala vizuri, na kumwezesha mtaji wa kufanyia kazi.”

Sentesi hiyo inamaanisha kuwa, Diamond anatimiza wajibu wake na tayari amempa mtaji mpenzi wake. Kuna taarifa pia kuwa hata filamu yake ya Family aliyoigiza na Aunty Ezekiel ilidhaminiwa na Diamond.

“Waswahili wanasema mchungaji bora anatakiwa kuhakikisha anampeleka ng’ombe wake kwenye maji safi, ila yeye ng’ombe mwenyewe ndio anatakiwa aamue kunywa maji,” anaendelea Diamond. “Au mnataka nikishampa mtaji niache kufanya na show tena na kuigiza nimuigizie mie ? Nisiende studio nikae dukani nimuuzie mie? Ni juhudi zako kwanza.”

Maneno ya Diamond yanajielezea yenyewe kuwa Wema amejisahau. Maswali ya wengi ni kuwa wao kama wapenzi hawajawahi kuzungumza haya na kushauriana? Diamond hajawahi kumkanya mpenzi wake kuwa mwenendo wake sio? Au ameshamuambia hadi amechoka na ndio maana ameamua kuuambia umma kile kinachoendelea?

Kwa lawama na matusi ambayo Diamond ameyapata kutokana na kampeni hiyo, ilikuwa inahitaji uvumilivu wa hali ya juu kukaa kimya. Nahisi uvumilivu ulimshinda na ndio maana aliamua kuandika alichokiandika ambacho bahati mbaya kinaweza kutia tena doa uhusiano wao. Sijui Wema atasemaje!!

 BONYEZA HAPA KUHUNGANA NA BLOG HII UPATE HABARI KIRAISI 

Taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu ugonjwa wa Ebola kuingia Tanzania.

Ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa umeingia kwenye headlines za dunia kutokana na kuripotiwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika sasa umeingia kugusa vichwa vya habari na kuihusisha Tanzania.

Waziri wa Afya wa Seif Rashid amesema wagonjwa waliohisiwa kupata maambukizo hayo kutokana na dalili za awali ni kutoka Benin na Mtanzania lakini baada ya vipimo wameonekana hawana maambukizo hayo.

Waziri Seif Rashid amesema kuwa tayari eneo maalumu limetengwa kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wagonjwa wanaotiliwa shaka kuwa na ugonjwa huo ikiwa ni kauli iliyotoka baada ya kufanyiwa uchunguzi kwa wagonjwa wawili waliohisiwa.

Kupitia ukurasa wake wa facebook, Waziri Seif amesema vifaa maalumu vitakavyotumiwa na watoa huduma katika kuhudumia wagonjwa vimewekwa pia huku wizara ya afya ikiongeza uwezo wa kufanya uchunguzi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere ambao wasafiri wengi kutoka nje huutumia.

Na mdadiblog/festosaimon
 ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG HII ILA TUNAOMBA UJIUNGE NASI KWA KUBONYEZA HAPA 

BEKI MPYA SIMBA APEWA NYUMBA MIKOCHENI

Wakati Coastal Union wakiendelea kumlilia beki Abdi Banda, mchezaji huyo ambaye amesaini mkataba wa kuichezea Simba, amepewa nyumba ya kuishi.

Hatua hiyo imekuja siku chache tangu mshambuliaji wa Simba, Mrundi Pierre Kwizera, kupewa nyumba ya kuishi pia maeneo ya Kunduchi.

Banda amepewa jumba eneo la Mikocheni huku ikikumbukwa kuwa enzi za utawala wa Mwenyekiti Ismail Aden Rage mchezaji aliyeishi sehemu za gharama kubwa alikuwa ni straika Amissi Tambwe ambaye alipangishiwa mitaa ya Sinza.

“Mimi si mwenyeji wa Dar, viongozi wameniambia kuwa tayari wamenitafutia nyumba Mikocheni na ndani ya wiki hii ninaweza kuhamia,” alisema Banda.

Unazikumbuka movie za Bad Boys 1& 2, hii ni taarifa mpya kuhusu movie hizo

Martin Lawrence na Will Smith ndio mastaa wa movie hizi mbili ambazo zina action na comedy ndani yake. Kama wewe ni mpenzi wa hizi movie basi taarifa ikufikie kwamba Bad Boys 3 ipo kwenye maandalizi.

Akiwa kwenye interview ya TV show actor Martin Lawrence aliulizwa kuhusu plan za movie ya Bad Boys 3 ambayo imekuwa kwenye tetesi kwa muda mrefu na Martin alijibu,”Nimeongea na director jana tu na ameniambia wanafanyia kazi script hivi sasa na wanakaribia kuimaliza.

Hivi karibuni mtapata taarifa rasmi ” Martin hakuthibitisha uhusika wa star mwenzake Will Smith kwenye hiyo movie kwasababu ni bado mapema sana

PHIRI APAA NA SKWADI ZIMA LA SIMBA SC ZENJI LEO, WAKIRUDI HUKO SASA…

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM BAADA ya kocha Mzambia Patrick Phiri kusaini Mkataba wa mwaka mmoja jana, kikosi cha Simba SC kinakwenda kambini visiwani Zanzibar leo kuweka kambi rasmi ya kujiandaa na msimu.

Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameambia mdadisiblog jana kwamba, kikosi kinaondoka asubuhi ya leo kwenda Zanzibar na kitarejea siku chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu na ratiba itatoka wiki moja kabla.

Tayari SImba SC imekamilisha usajili wake na wachezaji wote walikuwa wanahudhuria mazoezi mjini Dar es Salaam.

Phiri amerejea Simba SC baada ya miaka minne tangu aondoke mwaka 2010, akirithi mikoba ya Mcroatia Zdravko Logarusic aliyetupiwa virago mwishoni mwa wiki. Haijulikani mshahara wa Phiri utakuwa kiasi gani, lakini mara ya mwisho aliondoka Simba SC akiwa analipwa dola za Kimarekani 5,000 (zaidi ya Sh. Milioni 7.5) kwa mwezi.

Kocha huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2009/2010, aliyezaliwa Mei 3 mwaka 1956, alifanya kazi kwa awamu tatu tofauti akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kati ya mwaka 2004 na 2010 kwa mafanikio makubwa- na sasa anataka kurejesha enzi za wana Simba ‘kutembea vifua wazi’.

Mzambia huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba SC, misimu ya 2004/2005 na 2009/2010 na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 la Tanzania na Kenya.

Phiri ni kocha anayekubalika zaidi mbele ya mashabiki wa Simba SC miongoni mwa makocha waliowahi kufundisha klabu hiyo- rekodi yake ya kukumbukwa zaidi ikiwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009/2010 bila kufungwa hata mechi moja.

Lakini pia, namna alivyoweza kuiongoza Simba SC kuwatambia watani wa jadi, Yanga SC ni jambo lingine linalomfanya awe kocha mwenye heshima ya kipekee Msimbazi. Katika awamu zote tatu alizofundisha Simba SC awali, Phiri hajawahi kufukuzwa- kwani amekuwa akiondoka mwenyewe kwa sababu mbalimbali.

Phiri ni kocha mwenye mafanikio tangu anacheza soka katika klabu za Rokana United (sasa Nkana F.C.) na Red Arrows zote za nyumbani kwao, Zambia kama mshambuliaji.
Alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na 1982, kabla ya kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana.

Akiwa kocha, Phiri pia aliiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia kucheza Fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia nchini Nigeria mwaka 1997 kabla ya kushinda tuzo ya kocha bora wa mwaka nchini mwake mwaka 1999.

Simba SC Jumapili ilivunja mkataba na Mcroatia, Zdravko Logarusic ikiwa ni siku moja tu baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Loga ambaye aliongezewa Mkataba wa mwaka mmoja mwezi uliopita- inadaiwa amefukuzwa kwa sababu za kutotii miiko na maadili ya klabu na Rais Aveva alisema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kumvumilia kwa kiasi cha kutosha.

Loga ameondoka Simba SC baada ya kuiongoza katika mechi 21 tangu Desemba mwaka jana, kati ya hizo akishinda nane, sare tano

Na mdadisiblog/festo saimon
 ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG HII ILA TUOMBA UJIUNGE NASI KWA KUBONYA HAPA 

NAYE AGUERO AJITIA KITANZI KIZITO MAN CITY

Bado yupo sana Etihad: Sergio Aguero amesaini mkataba mpya Manchester City wa miaka mitano

KLABU ya Manchester City imewekeza jumla ya Pauni Milioni 175 kikosini make ndani ya siku nne, kufuatia mshambuliaji Sergio Aguero kuaini Mkataba mpya wa miaka mitano na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England Alhamisi usiku.

Mshahara mpya wa Aguero wa Pauni 150,000 kwa wiki umethibitishwa baada ya kusainishwa pia mikataba mipya kwa kiungo David Silva na beki Vincent Kompany ambao watadumu Etihad hadi mwaka 2019.

City iliianza wiki kwa kutoa Pauni Milioni 32 kumsajili beki wa FC Porto, Eliaquim Mangala anayeweka rekodi ya beki ghali katika historia ya soka ya Uingereza.
Na mdadisiblog/festo saimon

 ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG YETU ILA TUNAOMBA UJIUNGE NASI KWA KUBONYEZA HAPA 

MWANASHERIA NA WAKILI MAARUFU MBEYA APANDISHWA KIZIMBANI.

Picha na Rashid Mkwinda Blog WAKILI wa kujitegemea mkoani Mbeya na mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Taifa (MNEC) Sambwee Sitambala (42)amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu mkazi Mfawidhi wilaya ya Mbeya akituhumiwa kwa makosa mawili.

Shitambala amepandishwa jana akituhumiwa kwa makosa ya kuingia kwa jinai na kujenga nyumba katika viwanja viwili namba 27 na 28 Block BB lililopo eneo la Gombe Uyole Jijini Mbeya.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Gilbert Ndeuruo, wakili wa serikali, Ahmed Stambuli, alisema kuwa Shitambala anashitakiwa kwa kosa la kuingia kwa jinai kinyume cha kifungu namba 79 ya mwaka 2014 cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Alisema kuwa mshitakiwa kwa nyakati tofauti kati ya Juni 18, 2012 na Novemba 28, 2013 aliingia na kujenga katika viwanja namba 27 na 28 ambavyo vinadaiwa kuwa ni mali ya raia wa Tanzania mwenye asili ya kiasia aliyefahamika kwa jina la Jaswinder Palsingh.

Alisema kulingana na mazingira hayo, mshitakiwa amesababisha maudhi kwa mmiliki wa kiwanja hicho Palsingh na hivyo kushitakiwa kwa kosa la jinai. Shitambala ambaye alikuwa akitetewa na Wakili wa kujitegemea Tasco Luambano alikana shitaka hilo ambapo Hakimu Ndeuruo alisema kuwa dhamana ya Mshitakiwa iko wazi ikiwa atatimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja na ahadi ya fedha kiasi cha sh. milioni 1.

Kwa upande wake wakili wa serikali Stambuli alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba iko tayari kuanza kusikilizwa na kuiomba mahakama ipange tarehe ya kuanza kuisikiliza kesi hiyo.

Hakimu Ndeuruo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10 ambapo itaanza kusikilizwa rasmi.

Akizungumza nje ya mahakama mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo Wakili anayemtetea Shitambala,Luambano alisema kuwa kesi hiyo imefika hapo kutokana na maslahi ya baadhi ya watu na kuwa kisheria kesi za aina hiyo zinapaswa kusomwa katika mahakama ya Ardhi.

Alisema kuwa mteja amejenga katika eneo ambalo wamejenga watu wengine wapatao 400 na kuwa hata hivyo kesi hiyo imemhusu mteja wake pekee hali ambayo inaonesha nia mbaya iliyofanywa na mlalamikaji dhidi ya mteja wake.

Na mdadisiblog/festo saimon