Saturday, August 23, 2014

Simba inatia raha, Phiri amchezea akili Maximo

KOCHA mwenye heshima kubwa ndani ya Simba na ambaye amekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu hiyo msimu ujao, Mzambia Patrick Phiri, ametumia Mwanaspoti kuwaambia mashabiki wa timu hiyo kwamba washushe pumzi mambo ni mazuri. Amewasisitiza kwamba wasiwe na wasiwasi kwa vile kila kitu kipo sawa na heshima lazima irudi Msimbazi kwani ratiba ya Ligi Kuu Bara ameshaipata na wala haimsumbui. Katika mazoezi ya jana Ijumaa yaliyofanyika Uwanja wa Chuoni Chukwani, Phiri alisema wachezaji wake wanapokea kwa kiasi kikubwa mafunzo yake na anapenda kuona wanavyomiliki mipira, kukaba na kushambulia. Alichofanya jana ni kuwapunguzia muda wa mazoezi ambayo awali alikuwa akitumia saa nne na sasa anatumia saa tatu ili wapate muda wa kutafsiri mafunzo yake kambini na kutuliza akili. “Nafurahi kwa sababu naona wachezaji wananielewa kila ninachokihitaji, inanipa moyo sana kwamba msimu ujao tutafanya vizuri, nimetumia muda mwingi kuwafundisha jinsi ya kumiliki mipira, kukaba na kushambulia, kesho (leo Jumamosi) watafanya kidogo tu ili mwili ukae sawa tayari kwa mechi ya Jumapili dhidi ya Kilimani City (ya Daraja la Pili Zanzibar),” alisema Phiri. Akizungumzia maandalizi yake ya Ligi Kuu, alisema kuwa ameiona ratiba na mpangilio wake ni mzuri kwani watacheza mechi nyingi nyumbani katika mzunguko wa kwanza ila amesisitiza mechi yenye presha kuwa ni dhidi ya Yanga itakayochezwa Oktoba 12 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. “Ratiba imepangwa vizuri, tunatakiwa kushinda mechi zote lakini kwa uelewa wangu katika Ligi hii ya Tanzania mechi ya Yanga ina presha kubwa kwani ina mambo mengi sana hata kabla ya mechi kuchezwa, lakini tutajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Phiri. AMCHEZEA AKILI MAXIMO Katika kile ambacho ni kuonekana kumchezea akili kocha wa Yanga, Marcio Maximo, kama wanavyofanya makocha mahiri wa Ulaya, Phiri amedai kukerwa na ujio wa Yanga mjini Unguja. Yanga ilikuwa kambini Pemba lakini leo Jumamosi inatua Unguja na Kesho itacheza na KMKM kwenye Uwanja wa Amani. Phiri amedai hajafurahia Yanga kuamua kucheza mechi hiyo dhidi ya KMKM siku ambayo wao wana mechi katika uwanja huo wa Amani, mechi ya Yanga itaanza saa 10:00 jioni wakati ya Simba itaanza saa 2:30 usiku dhidi ya Kilimani. Phiri aliliambia Mwanaspoti kwenye kambi ya timu hiyo mjini hapa akisema: “Najaribu kuangalia itakuwaje kwani sisi ndio tumeanza kuja hapa na kutoa taarifa kuwa siku ya Jumapili tutakuwa na mechi, iweje Yanga nao wanataka wacheze siku hiyo hiyo? Kama uwanja usingekuwa mmoja hapo sawa, lakini nao wanataka kucheza uwanja ambao tutautumia.Credit mwanaspoti

Habari zingine za michezo BONYA HAPA 

0 comments:

Post a Comment