Thursday, July 17, 2014

SIMBA YANASA STRAIKA WA MAANA WA APR


STRAIKA Jean-Claude Iranzi wa APR ya Rwanda, amekubali kujiunga na Simba kwa dau la Dola 15,000 sawa na Sh.24 milioni tu na sasa anasubiri kuwekewa fesha hizo mezani ili amwage wino Msimbazi.

Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, amemkataa straika Daniel Mbukelo Van Wyk wa Afrika Kusini kwa kusema ana umri mkubwa na siye na jipya kwa timu yake.

Ni hapo ndipo uongozi wa timu ukaamua kufanya mazungumzo na Iranzi ambaye pia huichezea timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ na kufikia makubaliano hayo.

Iranzi amelihakikishia Mwanaspoti kuwa, ameshafanya mazungumzo ya awali na Simba na kilichobaki ni kutimizwa makubaliano ili aweze kujiunga na Wekundu wa Msimbazi hao kwa ajili ya kusaidiana na Amissi Tambwe kuzifumania nyavu za wapinzani.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Kigali kwa njia ya simu jana Jumatano, Iranzi alisema: “Nimeshafanya mazungumzo na Simba lakini nimewaomba wanisubiri mpaka nimalize mechi ya kufuzu Kombe la Afrika (Afcon) na timu yangu ya taifa.”

Iranzi yupo katika kikosi cha Rwanda kitakachocheza na DR Congo Jumapili jijini Kigali.

Iranzi mwenye umri wa miaka 22, alisema anaamini akisajiliwa na Simba atatoa ushirikiano mkubwa kwa wachezaji wenzake ili kuiletea mafanikio timu hiyo ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara na kurudia enzi zake za kutamba Afrika Mashariki.

“Hapa nasubiri mechi ya Rwanda ipite ili niendelee na mazungumzo na Simba halafu tumalizane,” alisema Iranzi.

Habari kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Simba zilisema kuwa, bado wanaendelea na mchakato wa kumnasa Iranzi baada ya Raphael Kiongera wa KCB ya Kenya kupandisha dau kutoka dola 15,000 mpaka 20,000 hivyo kuamua kuachana naye.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema Iranzi naye ametaka kiasi hicho cha fedha ambapo wamemuahidi kumpa endapo watafikia makubaliano.

“Ni kweli kuna kitu kama hicho lakini bado hatujamalizana, niliwaomba wanisubiri nimalize jukumu langu na timu ya Taifa ndipo tumalizane, ila sioni kama kuna tatizo mimi kucheza Simba, kwani ni timu kubwa na ni nzuri,” alisema Iranzi nayecheza kwa kutumia zaidi mguu wa kushoto.

Hata hivyo, kulikuwepo na mapendekezo ya majina mawili ya washambuliaji kutoka Nigeria endapo tu watashindwa kunasa sahihi ya mshambuliaji huyo.

Kama bado ujaungana na mimi kwenye facebook ili nikipata  habari zikufikie kirahisi
BONYEZA HAPA 


UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon

0 comments:

Post a Comment