RAIS mstaafu wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amekabidhi ofisi rasmi jana na kuwaasa wanachama 69 wa klabu hiyo waliokwenda mahakamani, kufuta kesi hiyo na kurudi kuzungumza na viongozi wao.
Aidha, amemsihi Rais wa sasa, Evans Aveva kufanyia kazi kauli yake aliyotoa kwenye kampeni ya kurudisha umoja kwa wanachama, kwa kuanza kuwasamehe waliokwenda mahakamani ili kuwa kitu kimoja.
Katika makabidhiano yaliyofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya klabu Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Rage alikabidhi Katiba ya Simba, mikataba ya TBL, Posta, Push Mobile, hati miliki za Jengo la ofisi hizo, Simba TV, mkandarasi wa Uwanja wa Bunju, mkataba wa madai ya fedha zao katika timu ya Etoile du Sahel wa kumuuza Em manuel Okwi, madeni na akaunti.
“Nakumbuka viongozi wote kila mmoja mliahidi kuleta umoja Simba, napongeza pia kuwa mliwasimamisha wale wanachama 65 (ni 69) waliokwenda mahakamani kuinusuru Simba, naamini katika mkutano wenu ujao nitasikia umewasamehe ili kuanza kurasa upya,” alisema Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika hilo, Rais mpya Aveva alisema analichukulia kama changamoto na kuahidi kuwa atakaa na Kamati ya Utendaji kuona kama watamalizaje.
Wakati Rage akikabidhi Katiba, alisema ni kwa ajili ya kumpa mamlaka ya kuitisha vikao vyote vya klabu kwa maendeleo huku akidai kuwa Urais hauna ubia, unahitaji kuendeshwa kwa kufuata maelekezo.
Kuhusu uwanja wa Bunju, alisema tayari wamelipa Sh milioni 80 kwa ajili ya kukamilisha uwanja huo na gharama iliyobaki ni Sh milioni 10 hivyo kuuomba uongozi huo kumalizia.
“Eneo ni karibu ekari 19 niliacha wanaweka majani baada ya kuota wataweka magoli, ni kitega uchumi kizuri, mnachotakiwa mfanye mtafute wawekezaji kwa ajili ya kufungua maduka, mtazalisha pesa nyingi,” alieleza Rage ambaye hakuwania kiti nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Juni 29, mwaka huu.
Kwa mkataba wao na Benki ya Posta Tanzania (TPB), alimtaka Aveva ajitahidi kutafuta mashabiki 50 Tanzania nzima ambao watakuwa wakichangia fedha kwa mwezi Sh 1,000 ili kufikisha jumla ya Sh milioni 50 kwa miezi sita ambazo zitasaidia kwa kiasi fulani.
Kuhusu akaunti, Rage alikataa kuweka wazi kwa madai kuwa walifanya kikao cha siri na uongozi huo mpya na kukubaliana kutoweka wazi kwani ni silaha kwa klabu.
Kwa upande wa madai ya Etoile, alisema hajapokea kiasi chochote, na kwamba wakati ule walimuuza Okwi kiujanja kwani hawakutaka kwenda kwenye klabu hiyo bure, hivyo alikabidhi mikataba kwa Aveva ili aendelee kufuatilia fedha hizo za mauzo Dola za Marekani 300,000.
Okwi kwa sasa anachezea Yanga. Yote yaliyofanywa na Rage, Aveva ameahidi kuendeleza pale alipoishia kwa manufaa ya klabu hiyo.
Kama bado ujalike ukurasa wetu wa facebook BONYEZA HAPA
UKIONA TUKIO LOLOTE USISITE KUTUTUMIA PICHA WHATSAPP NO:06570352125 Festo saimon







0 comments:
Post a Comment