Na Issa Ahmada, MOROGORO
YANGA SC imeanza kwa kipigo cha mabao
2-0 Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
kutoka Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro mshambuliaji Genilson Santana
‘Jaja’ akikosa penalti.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa
Dominick Nyamisana wa Dodoma,
aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha wa
Mwanza na Milambo Tshikungu wa Mbeya,
hadi mapumziko tayari Mtibwa Sugar
walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wa
zamani wa Simba SC na DC Motema Pembe
ya DRC, Mussa Hassan Mgosi dakika ya 16
aliyemalizia pasi ya kichwa ya Ame Ali na
kumuwahi kipa Deo Munishi ‘Dida’
aliyetokea vizuri kutaka kudaka.
Baada ya bao hilo, nyuki wakaingia uwanjani
jambo lililosababisha wachezaji walale chini
kwa dakika mbili, kabla ya wadudu hao
kuondoka na mchezo kuendelea.
Almanusra Genilson Santana ‘Jaja’
aisawazishie Yanga SC dakika ya 32 baada
ya kuunganisha vizuri kwa kichwa kona ya
Haruna Niyonzima, lakini Hassan Ramadhani
akauokoa ukiwa unaelekea nyavuni.
Dakika ya kwanza tu ya kipindi cha pili,
Yanga SC walipata penalti baada Salim
Mbonde kuunawa mpira kwenye eneo la
hatari, lakini kipa Said Mohamed Kasarama
akapangua kwa mguu mkwaju wa Jaja.
Dakika ya 47, Simon Msuva aliyetokea
benchi kuchukua nafasi ya Hamisi Kiiza
‘Diego’aliifungia Yanga SC bao, lakini refa
akasema aliotea. Dakika ya 49 tena, Mrisho
Ngassa alifunga bao lakini refa akasema
aliotea pia.
Dakika ya 67, Simon Msuva alivamia langoni
mwa Mtibwa na kutoa vitu vilivyokuwa chini
upande wa nyavu kubwa na kukimbia navyo
huku akikimbizwa na kipa Said Mohamed
Kasarama kabla ya kuvitupa nje.
Dakika ya 82 mpishi wa bao la kwanza, Ame
Ali aliifungia Mtibwa bao la pili baada ya
kufanikiwa kuwahadaa mabeki wawili wa
kati wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannaaro’
na Kevin Yondan kisha kumtungua Dida
kufuatia pasi nzuri ya Hassan Ramadhani.
Yanga SC iliathiriwa na mabadiliko
iliyoyafanya dakika za mwishoni kumtoa
Mbuyu Twite aliyekuwa mhimili wa safu ya
ulinzi na kuingiza mshambuliaji, Said
Bahanuzi.
Kocha wa Yanga SC, Marcio Maximo
ambaye alimfundisha kocha wa Mtibwa
Sugar, Mecky Mexime alipokuwa Taifa Stars
alikuwa mnyonge baada ya meci hiyo.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Said
Mohammed, Hassan Ramadhani, David
Luhende/Majaliwa Shaaban dk64, Salim
Mbonde, Andrew Vincent, Shaaban Nditi, Ali
Shomary, Muzamil Yassin, Ame Ali, Mussa
Mgosi/Vincent Barnabas dk50 na Mussa
Nampaka/Dickson Daud dk72.
Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul,
Oscar Joshua/Omega Seme, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite/
Said Bahanuzi dk72, Hassan Dilunga,
Haruna Niyonzima, Genilson Santana ‘Jaja’,
Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/Simon
Msuva dk46. |
0 comments:
Post a Comment